1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Rais Macron kumtangaza waziri mkuu mpya wa Ufaransa

13 Desemba 2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, anatarajiwa kumtangaza waziri mkuu mpya wa nchi hiyo leo Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4o5ag
PICHA YA MAKTABA | Emmanuel Macron
Yeyote ambaye Macron atamchagua, atakuwa waziri mkuu wa sita tangu Macron alipochukua hatamu za kuiongoza UfaransaPicha: LUDOVIC MARIN/Pool/REUTERS

Ni kulingana na wasaidizi wake baada ya siku kadhaa za mkwamo wa kumtafuta mgombea wa kuchukua nafasi ya Michel Barnier ambaye kuondolewa kwake madarakani na bunge kupitia kura ya kutokuwa na imani naye, kumeiingiza Ufaransa katika mgogoro mpya.

Msaidizi mmoja wa rais aliyezungumza jana jioni kwa sharti la kutotambulishwa muda mfupi baada ya Macron kurejea nchini humo kutoka Poland, amesema taarifa ya kumtangaza waziri huyo mkuu mpya itachapishwa leo asubuhi.

Msaidizi huyo pia amesema Rais Macron yuko katika harakati za kumaliza mashauriano yake, lakini hakutoa maelezo zaidi.

Yeyote atakayechaguliwa, atakuwa waziri mkuu wa sita chini ya uongozi wa Macron baada ya kuondolewa madarakani kwa Barnier, ambaye alihudumu kwa miezi mitatu pekee.