1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Magufuli atoa tahadhari ya uvaaji wa barakoa kutoka nje

22 Februari 2021

Kwa mara ya kwanza, Rais John Magufuli wa Tanzania ametamka kuwa serikali yake haijapiga marufuku uvaaji barakoa ila amesisitiza barakoa zinazotoka nje ya nchi zisiaminike.

https://p.dw.com/p/3pgp8
Tansania Dar es Salaam | Trauer um John William:  Präsident John Magufuli leitet Trauerveranstaltung
Rais wa Tanzania John Magufuli akiwaongoza viongozi wengine serikalini katika maziko ya Katibu Mkuu wa Balozi John William Kijazi mjini Dar es Salaam Picha: Said Khamis/DW

Kuhusu uvaaji wa barakoa, Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza katika ibada kanisani, amesema serikali yake haijachukua uamuzi wa kuzipiga marufuku ila anachosisitiza ni watu kuondokana na hofu badala yake kumtegemea mwenyezi Mungu.

Amesema haamini janga hilo ni hatari kushinda mapenzi ya Mwenyezi Mungu na akiwataka pia watanzania kuendelea kutumia njia za asili kama vile ufukizaji ili kujilinda na maambukizi ya virusi hivyo vya corona.

soma zaidi: Tanzania yazipiga marufuku taasisi kuzungumzia Corona

Tangu kuibuka kwa kile kinachofahamika wimbi la pili la maambukizi ya virusi hivyo, kumekuwa na maoni mengi kuhusu matumizi ya barakoa huku makanisa yakiweka msimamo wake bayana unaopendelea kuona waumini wake wakichukua tahadhari  kubwa.

Wengi waendelea kufa kwa kile kinachodhaniwa ni kutokana na COVID 19

Tansania Dar es Salaam | Trauer um John William:  Präsident John Magufuli leitet Trauerveranstaltung
Makamu wa rais Tanzania Bi Samia Suluhu akiwafariji wafiwa katika maziko ya Katibu Mkuu Balozi John William Kijazi mjini Dar es Salaam Picha: Said Khamis/DW

Ingawa kwa wakati huu viongozi wa serikali wamekuwa wakisisitiza uchukuaji wa tahadhari, lakini makisa hayo ikiwamo kanisa katoliki ndilo linaloonekana kuweka msimamo wa wazi kuhusiana na matumizi ya barakoa hizo.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa ibada moja, askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, askofu Thaddeus Ruwa'ichi alionekana kuvunjika moyo na wale wanaokwenda kwenye ibada huku wakiwa hawana barakoa yoyote.

soma zaidi: Maalim Seif azikwa Pemba

Katika hatua nyingine, wananchi wa Tanzania wameamka na majonzi mengine kufuatia kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Profesa Beno Ndulu aliyeaga dunia leo afajiri akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kairuki iliyoko jijini Dar es salaam.

Msomi huyo wa uchumi ambaye pia amewahi kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kuwahi kufanya kazi katika Benki ya Dunia ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 71. Hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuelezea sababu ya kifo chake.

Alikuwa gavana katika benki kuu katika kipindi cha kuanzia January 2008 hadi alipomaliza muda wake mwaka 2018. Katika siku za hivi karibuni Tanzania imekuwa ikishuhudia ongezeko la vifo ikiwamo vile vinavyowahusisha watu waliowahi kushika nyadhifa kubwa serikalini.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam