Rais Mugabe awekwa katika kizuizi cha nyumbani
15 Novemba 2017Hali ya wasiwasi imeendelea kuukumba mji wa Harare Zimbabwe, huku vifaru vya kijeshi pamoja na wanajeshi wakipiga doria katika mitaa ya mji huo pamoja ana kulinda ofisi za serikali. Hali bado ni ya wasiwasi.
Jeshi la Zimbabwe limesema limechukua udhibiti wa mamlaka lakini limekana kuwa hatua yao ni mapinduzi bali ni kuwalenga wahalifu walio karibu na rais. Baada ya kuzungumza na rais Mugabe, rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema Mugabe yuko katika kizuizi cha nyumbani nyumbani chini ya ulinzi wa kijeshi.
Familia ya rais haijaonekana hadharani tangu mzozo huo kuanza, hali ambayo imeibua swali la wapi aliko mkewe rais, bibi Grace Mugabe.
Zuma atuma ujumbe
Zuma amesema ametuma ujumbe kuzungumza na viongozi wa kijeshi ambao wamefanya operesheni hiyo, na pia Rais Mugabe ili kupata taswira kamili ya kile kinachofanyika nchini humo. Aidha alisema atatuma ujumbe kwa rais wa Angola Joao Lourenco ambaye ni mwenyekiti wa Idara ya uasalama na amani ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika -SADC, kumueleza kuhusu hali ya amani na utulivu ili kuwe na mahusiano ya karibu baina yao na Zimbabwe.
Zuma ameongeza kuwa: "Ninatumai kuwa jeshi halitasababisha uharibifu zaidi, na kwamba wataheshimu katiba ya Zimbabwe na raia wake ili hali hii isipindukie ilipo kwa sasa haswa kwa kuwa tunawasiliana na jeshi pamoja na rais Mugabe mwenyewe. Tunatumai hali hii itadhibitiwa ili Amani na utulivu urejee Zimbabwe."
Maveterani wataka Mugabe aondolewe madarakani
Katibu Mkuu wa chama cha taifa cha maveterani wa vita Victor Matemadanda amesema Rais Mugabe ambaye pia ndiye kiongozi wa chama tawala cha Zanu-PF anapaswa kuondolewa madarakani, na kwamba kunastahili kuwepona tume ya uchunguzi kuchunguza uhalifu aliofanya wakati wa uongozi wake. Matemadanda yuko karibu wa jeshi na aliyekuwa makamu wa rais Emmerson Mnangagwa aliyefutwa kazi wiki iliyopita ameendelea kusema "tunahimiza kwamba wakati baraza kuu linapokutana, linapaswa kwa haraka kuitikia wazo la kuwa na ligi ya maveterani wa vita kama tawi la nne la chama cha mapinduzi."
Wito wa suluhisho la amani
Umoja wa Ulaya umetoa wito wa suluhisho la Amani kwa mzozo wa Zimbabwe. Msemaji wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Catherine Ray amesema hali ya Zimbabwe inawatia wasiwasi na kwamba wanazitaka pande zote husika kuepuka makabiliano, badala yake wazungumze kwa lengo la kupata suluhisho la Amani. Bibi Catherine ameongeza kuwa wanafuatilia kwa karibu yanayofanyika na wanatilia uzito haja ya kuhakikisha haki za kimsingi za raia zinaheshimiwa na katiba pamoja na utawala wa kidemokrasia unadumishwa.
Uingereza nayo imesema hali haiko wazi ikiwa hatua ya jeshi kudhibiti mamlaka inaashiria kufeli kwa rais Mugabe. Akitoa wito kwa raia wa Uingereza walioko Zimbabwe kusalia majumbani mwao na kufuatilia matukio kwa karibu, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Johnson Boris amesema hawajui jinsi hali itakavyokuwa katika siku zijazo.
Zimbabwe imeendelea kuwa chini ya udhibiti wa kijeshi siku mbili baada ya mkuu wa jeshi kumuonya Rais Robert Mugabe dhidi ya kuwatimua wakuu wa chama tawala. Wachambuzi wanasema inaonekana ni kilele cha mvutano wa madaraka kati ya wakuu waliopigania mapinduzi ambao wanamuunga mkono makamu wa rais aliyefutwa kazi wikiiliopita Emmerson Mnangagwa na vikosi vitiifu kwa mke wa rais bibi Grace Mugabe.
Mugabe na mke wake Grace wako katika orodha ya waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: John Juma/AFPE/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman