Rais Museveni azusha gumzo, lini uchaguzi utafanyika Uganda?
29 Mei 2020Baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani wameyataja matashi ya rais huyo kuwa hila za kutaka kutumia kisingizio cha mripuko wa ugonjwa wa COVID-19 kung'ang'ania madarakani na kutumia kanuni za kudhibiti janga hilo kuudhoffisha upinzani.
Kulingana na rais Museveni kanuni zote ambazo ametangaza katika kipindi cha kupambana na kuenea kwa virusi vya COVID-19 zimetokana na ushauri wa wanasayansi na ndiyo maana Uganda imefanikiwa kuepusha kusambaa kwa ugonjwa huo hatari.
Vilevile wanawategemea wanasayansi kutoa ushauri bora kuhusu kipindi cha kampeni na uchaguzi mkuu wa mwaka 2021. Hoja hii imeibua mjadala mkubwa katika kongamano la vyama vya kisiasa linaloendelea wiki hii.
Baadhi wanakubaliana na mtazamo huo na kuongezea kuwa ingekuwa bora uchaguzi mkuu uahirishwe angalau kwa mwaka mmoja au miwili.
Upinzani wasema kuna hila
Hata hivyo wanasiasa wa upinzani wanaelezea kuwa katiba ya nchi lazima ifuatwe ila wanasayansi watoe ushauri kuhusu njia za kuendesha uchaguzi bila kusababisha maambukizi. Asuman Basalirwa ni mbunge wa upinzani.
Patrick Okoboi ambaye ni rais wa chama cha FDC pamoja na wanasiasa wengine wanasema kwa kuwa hakujatangazwa hali ya hatari nchini Uganda, mwongozo wa katiba bado unazingatiwa.
Mjadala wa kuahirishwa uchaguzi uliwahi kuibuka wakati janga la COVID-19 lilipobainika mapema mwezi Machi. Mtazamo wa baadhi wakati huo uliangazia kuepusha uchumi wa nchi kuporomoka kutokana na mfululizo wa mambo ambayo yangewasababisha wawekezaji na wajasiriamali kwa jumla kusita kuanzisha au kuongeza mtaji katika shughuli zao.
Uchaguzi huhusisha kampeni na hata maandamano ambayo husababisha mikusanyiko ya watu. Hii ni ikinyume na kanuni za kuepusha kuenea kwa virusi vya Corona.