Rais Musharaf anatazamiwa kulihutubia taifa leo au kesho
11 Julai 2007Vikosi vya usalama vya Pakistan vimekamilisha shughuli za kulisafisha eneo unakokutikana Msikiti Mwekundu mjini Islamabad,siku moja baada ya opereshini iliyogharimu maisha ya mkuu wa waasi Abdul Rashid Ghazi na wafuasi wake zaidi ya 50.Wanajeshi tisaa pia wa serikali wameuwawa.
“Opereshini imeshakamilika,zimesalia sehemu za mwisho mwisho tuu zinazosafishwa-na haitachukua muda mrefu” amesema jenerali Waheed Arshad,masaa 24 baada ya vikosi vya usalama kulivamia eneo hilo..
“Wamesalia wanamgambo wachache tuu” ameongeza kusema msemaji huyo wa jeshi aliyefafanua kwamba wanajeshi wameanza kuchunguza kama kuna miripuko au baruti zilizofichwa.
“Opereshini ya safisha safisha ni muhimu ili kuhakikisha eneo lote ni salama na linaweza kutembelewa bila ya shida na waandishi habari kwa mfano.Eneo lote hili linahitaji kusafishwa kwasababu tunataka kuhakikisha hakujaachwa miripuko au baruti zozote nyengine.”
Vikosi vya usalama vimesema kuna kundi la wanamgambo 12 tuu wanaoendelea kupigana.Wamejificha ndani ya mahandaki chini ya Madrasa.
“Wamekaa kama mapanya “amesema afisa mmoja wa ngazi ya juu wa kijeshi huku miripuko ikisikika hapa na pale sawa na risasi za rashasha kutoka jengo hilo.
Jenerali Arshad ametangaza vifo vya waasi watatu vilivyojiri usiku wa jana kuamkia leo na kuifanya idadi ya waasi waliouliwa kufikia watu 53.Wanajeshi tisaa wameuliwa pia.Vyombo vya habari vya Pakistan vimewanukuu maafisa wa serikali wanaozungumzia juu hasara ya maisha ya watu kati ya 80 na mia mbili.
“Patahitajika muda hadi idadi halisi ya watu waliouliwa itakapojulikana-amesema msemaji huyo wa jeshi na kuongeza tunanukuu:”maiti bado hazijaondoshwa.”Mwisho wa kumnukuu.
Idadi kubwa ya wahanga,na hasa kama wahanga hao ni wanawake na watoto inaweza kumtia mashakani rais Pervez Musharaf anaekabiliwa na kishindo kikubwa kuwahi kushuhudiwa tangu alipoingia madarakani miaka minane iliyopita.
Rais Pervez Musharaf anatazamiwa kulihutubia taifa leo usiku au kesho kutangaza mkakati mpya wa kupambana na magaidi.
Wananchi wa Pakistan wanaonyesha kuunga mkono uamuzi wa serikali wa kuwatimua wafuasi wa itikadi kali toka msikiti mwekundu.Hata hivyo wapinzani wake waliokusanyika mjini London wanaonya dhidi ya madhara yasiyokadirika ya kuvamiwa msikiti mwekundu mjini Islamabad.Wanaamini opereshini hiyo inaweza kupalilia itikadi kali nchini Pakistan.
Viongozi wa vyama vya upinzani waliokutana mjini London wamemtaka rais Musharaf ajiuzulu ,paundwe sereikali ya mpito na kuitishwa uchaguzi wa bunge haraka.