1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Rais Ramaphosa afanya ziara rasmi kasri la Buckingham

22 Novemba 2022

Mfalme Charles kwa mara ya kwanza amkaribisha rais wa Afrika Kusini katika ziara ya siku mbili ya kiserikali nchini Uingereza

https://p.dw.com/p/4JuBV
Großbritannien - Besuch von südafrikanischem Präsident Cyril Ramaphosa
Picha: Daniel Leal/AFP

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa leo Jumanne atakuwa mgeni katika kasri la mfalme Charles wa Uingereza,itakuwa ni mara ya kwanza mfalme huyo kupokea ugeni rasmi wa kiserikali tangu alipotawazwa mfalme .

Rais Ramaphosa na mkewe waliwasili jana Jumatatu nchini Uingereza lakini watapokelewa rasmi na mwanawe wa kwanza mfalme Charles,William  pamoja na mkewe, Kate leo Jumanne wakati akianza rasmi ziara yake ya siku mbili.

London King Charles III Empfang
Picha: Isabel Infantes/Avalon/Photoshot/picture alliance

Ziara hiyo itajumuisha makaribisho ya heshima yatakayofanywa na mfalme na mkewe Camilla na msafara maalum wa kifalme utakaozunguuka kwenye eneo la makaazi ya kifalme mpaka kwenye kasri la Buckingham ambako dhifa maalum itafanyika kumpa heshima rais huyo wa Afrika Kusini.

Ramaphosa pia atakwenda Westminster Abbey kuweka shada la maua katika kaburi alikozikwa  shujaa ambaye hakutajwa jina pamoja na kujionea  jiwe la kumbukumbu lililowekwa kwenye kanisa hilo kwa ajili ya kumkumbuka  rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela.

Großbritannien - Besuch von südafrikanischem Präsident Cyril Ramaphosa
Picha: Daniel Leal/AFP

Lakini pia rais huyo wa Afrika Kusini,Cyril Ramaphosa atalihutubia bunge  mjini London na kukutana na waziri mkuu Rishi Sunak.

Kwa mujibu wa waziri mkuu huyo anatarajia kujadiliana na rais Ramaphosa juu ya masuala kadhaa ikiwemo namna ya kuongeza ushirikiano kati ya mataifa yao pamoja na kutumia fursa zilizopo pande zote mbili  katika nyanja za biashara na utalii usalama na ulinzi.

 Ziara ya mwisho ya kiongozi wa Afrika Kusini nchini Uingereza ilifanywa mwaka 2010 na rais Jacob Zuma na walikutana na Charles na Camilla mwanzoni mwa ziara hiyo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW