Rais Touadera wa CAR azuru Moscow kuimarisha ushirikiano
16 Januari 2025Moscow ina mahusiano ya karibu na koloni hilo la zamani la Ufaransa, ambapo imepeleka nchini humo mamia ya kile wanachoita wanajeshi wa kutoa mafunzo ili kuisaidia serikali ya Touadera kupambana na makundi yanayozozana ya waasi.
Kama sehemu ya ziara yake ya siku tatu, Touadera anakutana na Rais Vladmir Putin siku ya Alhamisi kujadili hatua zaidi ya ushirikiano wa pande mbili.
Moscow imedhamiria kutanua ushawishi wake Afrika katika miaka ya karibuni, ikitoa msaada wa kiusalama kwa viongozi wanaozozana na kuibua hisia za chuki dhidi ya nchi za Magharibi.
Jamhuri ya Afrika ya Kati, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mamluki wa Urusi kutoka kundi la Wagner wamevisaidia vikosi vya serikali nchini humo tangu mwaka wa 2018, huku Moscow pia ikiwapa mafunzo maelfu ya askari wa nchini humo.