1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa China ziarani Mali

Oumilkher Hamidou12 Februari 2009

Hu Jintao aanza ziara yake barani Afrika hii leo

https://p.dw.com/p/Gsjt
Mji mkuu wa Mali,BamakoPicha: DW


Rais Hu Jintao wa China amewasili Mali hii leo,kituo chake cha kwanza cha ziara yake barani Afrika ambapo anatazamiwa kushadidia upya juu ya msaada wa nchi yake kwa nchi za Afrika,licha ya mgogoro ulipo wa kiuchumi duniani.


Kabla ya Senegal,Tanzania na Mauritius,ziara ya saa 24 ya rais huyo wa jamhuri ya umma wa China nchini Mali,imelengwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kutakasa njia ya miradi mengine.


Nchi kubwa yenye wakaazi milioni 14,Mali ni nchi ya tatu inayochimba dhahabu kwa wingi barani Afrika,baada ya Afrika kusini na Ghana na mojawapo ya nchi zinazosafirisha pamba kwa wingi duniani.Maadini ya Uranium yamegunduliwa pia hivi karibuni katika eneo la kaskazini la Mali linalokumbwa na uasi wa watuareg.


Katika bara hili linalozidi kumezewa mate kutokana na utajiri wake wa mali asili ambayo kwa sehemu kubwa haijatikisika hata kidogo,serikali ya mjini Bamako imegeuka kua mshirika wa kuaminika wa Beijing tangu uhuru mwaka 1960.


Tangu miaka 50 iliyopita,viongozi wote wa taifa wa Mali wameshafika ziarani mjini Beijing na rais Amadou Toumani Touré ameshakwenda mara zisizopungua tatu hadi sasa.


Wakati wa ziara hii ya sasa,marais hao wawili wataweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa daraja ya tatu ya mjini Bamako.Ujenzi wa mradi huo unagharimiwa kikamilifu na China kwa kitita jumla cha euro milioni 30.


Viongozi hao wawili watafungua pia kituo cha huduma za kinga na tiba dhidi ya homa ya Malaria katika hospitali ya Kati,umbali wa kilomita 15 toka mji mkuu Bamako.Kituo hicho pia kimejengwa kutokana na msaada wa fedha kutoka china.


"Uhusiano wa kiuchumi na kisiasa,wanasema wanaharakati wa haki za binaadam nchini Mali usiwe chanzo cha kutozungumziwa ukweli wa mambo."Hayo ni maoni ya mwenyekiti wa shirika la Amnesty International-tawi la Mali,Makan Koné anaesema:


"Haki za binaadam zinavunjwa nchini China.Lakini kwa bahati mbaya,uhusiano kati ya mataifa hautilii maanani upande huo."


Baada ya ziara yake nchini Mali,rais Hu Jintao atakwenda Senegal.Beijing na Dakar zimeanzisha upya uhusiano wa kibalozi mnamo mwaka 2005 baada ya uhasama wa miaka kumi uliosababishwa na uamuzi wa Senegal wa kuitambua Taiwan.


Baada ya ziara yake Afrika Magharibi,rais Hu Jintao ataitembelea Tanzania na baadae Mauritius.


Kiu cha Beijing kwa mali ghafi ya Afrika kimekosolewa na mataifa ya magharibi yanayoilaumu China kwa kutoshurutisha msaada wake au uhusiano wake na utawala bora au kuheshimiwa haki za binaadam.