Rais wa FIFA aridhishwa na Kombe la Mabara
19 Juni 2017Lakini kabla ya kuanza dimba hilo, kulikuwa na tetesi za hapa na pale kuhusiana na umuhimu wa michuano hiyo, na hata wengine walidai kuwa hii huenda ikawa awamu ya mwisho ya dimba hilo la mabara kabla ya kufutiliwa mbali. Lakini Rais wa FIFA Gianni Infantino ameeleeza kuridhishwa kwake na namna michuano hiyo ilianza Urusi mwishoni mwa wiki ijapokuwa hajazungumzia kuhusu mustakabali wake.
Akizungumza kabla ya mechi ya Chile na Cameroon, Infantino alisema dimba hilo limeanza kwa kasi inayostahili na kuwa mashabiki waliburudishwa na mchuano wa ufunguzi ambao wenyeji Urusi waliwalaza New Zealand mabao mawili kwa moja. Rais huyo wa FIFA anasema ni wakati wa kuzingatia kandanda lenyewe na sio kuzungumzia mustakabali wa dimba hilo
Mrundiko wa mechi una maana baadhi ya makocha wa kimataifa wanaamini kuwa kinyang'anyiro hiki kinachosha. Idadi ya mashabiki wanaofika viwanjani na kutizama kwenye televisheni ni ndogo kuliko michuano ya kiwango cha juu ndio maana hata haishangazi kuwaona mabingwa wa dunia Ujerumani wakipeleka timu ya pili isiyokuwa na wachezaji wengi vigogo
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo