Rais wa Haiti Jovenel asema hatajiuzulu
15 Februari 2019Rais wa Haiti Jovenel Moise kwa mara ya kwanza amevunja ukimya baada ya wiki ya maandamano ya kumshinikiza kujiuzulu, wakati Marekani ikitangaza kuwaondoa baadhi ya watumishi ambao hawahusiki na huduma za dharura nchini humo kufuatia machafuko hayo.
Kwenye hotuba yake kwa raia iliyorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha serikali, rais Jovenel amesema, hatokubali kuikabidhi nchi hiyo kwa magenge ya wanaomiliki silaha na wauza dawa za kulevya. Ametoa hotuba hiyo baada ya makabiliano kati ya mamlaka na raia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince.
Takriban watu 7 wameuawa na wengine kujeruhiwa kwenye machafuko hayo ya tangu Februari 7, yaliyoiingiza Haiti katika mzozo wa kisiasa. Amesema hatua kadhaa tayari zimeanza kuchukuliwa na serikali ili kukabiliana na machafuko zaidi nchini humo. Jovenel ameendelea kusema: "Tunawasilikiliza raia na hatua kadhaa tayari zimekwishachukuliwa na serikali. Nimemuomba waziri mkuu aje kuzielezea, lakini pia kuzitumia mara moja ili kupunguza matatizo yetu."
Awali, rais Jovenel aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter akiwataka raia kujizuia na machafuko, na kuitisha mazungumzo ili kusaka suluhu. Makundi ya upinzani hayako tayari kuingia katika mazungumzo hadi pale Moise atakapoachia madaraka.
Mmoja ya waandamanaji hao ambaye hakujitambulisha alililalama. "Niko katika hali hii kwa sababu ya rais Jovenel. Siwezi kwenda shule. Jovenel ni mwizi, ni lazima aondoke, kama sivyo tutaharibu kila kitu kwenye nchi hii. Tutakuwa mitaani hadi atakapoondoka."
Maandamano hayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kusimama kwa shughuli za kibiashara, shule na hata usafiri wa umma. Waandamanaji waliweka vizuizi vya moto na polisi walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji, ambao wengine walitumia mwanya huo kulidhibiti eneo la biashara, kuvunja maduka na kuiba mali.
Waandamanaji hao wanaituhumu serikali kwa ufisadi wakisema ilitumia vibaya ufadhili uliotolewa kupitia mkataba wa muungano wa mataifa ya Carribean na Venezuela wa PetroCaribe, uliokusudiwa kwa ajili ya ujenzi mpya wa taifa hilo baada ya kukumbwa na tetemeko baya la ardhi mnamo mwaka 2010, na kusababisha vifo vya hadi watu 300,000.
Kulingana na Benki ya Dunia, Haiti ni taifa masikini zaidi katika visiwa vya Marekani, ikiwa na asilimia 59 ya idadi jumla ya watu milioni 10.4 wanaoishi chini ya wastani wa kitaifa wa umasikini wa dola 2.41 kwa siku. Kumekuweko na ongezeko la mfumuko wa bei na raia wengi wakipambana hata kulipa gharama za huduma za msingi.
Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/RTRE
Mhariri: Josephat Charo