1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Rais wa Korea Kusini Yoon akataa kuhojiwa na wapelelezi

16 Januari 2025

Rais wa Korea Kusini aliyeachishwa madaraka na bunge Yoon Suk Yeol amekataa kuhojiwa tena na wapelelezi, siku moja baada ya kukamatwa kutokana na amri yake iliyoshindwa ya kutangaza sheria ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/4pCHn
Korea Kusini | Rais Yoon Suk Yeol anakabiliwa na mashitaka ya uasi
Rais Yoon Suk Yeol anakabiliwa na mashitaka ya uasiPicha: Yonhap/REUTERS

Mahakama ya Kikatiba pia imeanza kikao cha pili cha kusikiliza kesi hiyo siku ya Alhamisi. Kesi hiyo itaamua kama iuidhinishe uamuzi wa bunge wa kumvua madaraka Yoon au la.

Yoon ndiye rais wa kwanza aliyeko madarakani nchini Korea Kusini kukamatwa na polisi. Rais huyo, ambaye anakabiliwa na mashitaka ya uasi, alihojiwa kwa saa nyingi jana lakini akatumia haki yake ya kikatiba kusalia kimya kabla ya kupelekwa katika jela ya mjini Seoul.

Wapelelezi kutoka Ofisi ya Uchunguzi wa Rushwa walitarajiwa kuendelea siku ya Alhamisi kumhoji Yoon, lakini timu yake imesema hatohudhuria. Wakili wake amesema rais huyo hatohudhuria kwa sababu za kiafya.

Yoon alisema alishirikiana na wapelelezi ili kuepusha umwagaji damu lakini hakubaliani na uhalali wa uchunguzi huo.

Wakati huo huo, maafisa wanajaribu kupata waranti mpya ambao unaweza kuruhusu ashikiliwe kwa zaidi ya saa 48.