Rais wa Marekani ana nguvu kiasi gani?
4 Novemba 2020Rais huchaguliwa kushikilia kipindi cha miaka minne kwa mihula miwili tu. Anakuwa mkuu wa dola na pia mkuu wa serikali, akiwa ana udhibiti wa serikali kuu ambayo imeajiri takribani watu milioni nne, wakiwemo wanajeshi. Rais anawajibika kutekeleza sharia zinazopitishwa na bunge ama baraza la Congress. Na akiwa ndiye mwanadiplomasia wa juu kabisa wan chi, rais wa Marekani anaweza pia kuwapokea mabalozi wa mataifa mengine na kwa hivyo kuyatambua mataifa hayo.
Kuna matawi au mikono mitatu ya serikali, ambayo ni utawala wenye baraza la mawaziri chini ya rais, mahakama na bunge, na kwa pamoja matawi haya hushirikiana kufanya maamuzi, jambo ambalo kimsingi huzuwia nguvu za mkono mwengine. Kwa mfano, licha ya kwamba rais ndiye anayeweza kuwasamehe wafungwa na kuteuwa majaji wa mahakama ya juu, ni lazima maamuzi yake hayo yaridhiwe na Baraza la Seneti. Rais huwateuwa pia mabalozi na mawaziri, lakini nao pia lazima waridhiwe na Seneti. Hii ni njia mojawapo ambapo chombo cha kutunga sharia kinaudhibiti utawala wa serikali.
Kuna kitu pia kinaitwa hotuba ya ''Hali ya Muungano'', ambapo rais anatakiwa kuitowa katika kulifahamisha Baraza la Congress jinsi nchi inavyokwenda. Ingawa rais hawezi kuanzisha miswaada ya kisheria, anaweza kupitia hotuba hiyo kujadili mada na mikakati ambayo anataka kuona ikitekelezwa. Hii ni namna moja ya kuishinikiza Congress kufanya kazi, lakini hawezi kufanya zaidi yah apo.
Nguvu nyengine ya rais wa Marekani ni kupiga kura ya turufu dhidi ya mswaada wa sharia na kuurejesha Congress bila kuusaini. Lakini kura hii ya turufu inaweza kupinduliwa na thuluthi tatu ya wajumbe wa mabaraza yote mawili wa bunge la Marekani, yaani Baraza la Wawakilishi na Seneti. Hata hivyo, kwa mujibu wa Seneti, ni kura za turufu 111 tu kati ya 1,516 ndizo walizofanikiwa kuzipinduwa, yaani wastani wa asilimia 7 tu.
Kuna nguvu nyengine ambazo tunaweza kuziita nguvu za giza kwenye miliki ya rais wa Marekani. Katiba na maamuzi ya Mahakama ya Juu hayaelezi kwa ufasaha hasa kiasi gani rais ana nguvu kwenye eneo fulani. Ndiyo maana kuna kitu kinaitwa "turufu ya mfukoni”, ambayo humruhusu rais kuushikilia tu mswaada wa sharia bila kuusaini wala kuurejesha Congress na kwa hivyo kuufanya usifanye kazi. Pamoja na madaraka yake, Congress haiwezi kuipindua aina hii ya turufu. Nayo imeshatumiwa zaidi ya mara moja na marais mbalimbali wa Marekani.
Hata hivyo, kwa upande mwengine kuna amri za kawaida za rais lakini zinazofanya kazi kama sharia. Rais anaweza kuwaamuru wafanyakazi wa serikali kutekeleza jambo fulani kwa njia fulani na au kwa malengo fulani. Amri hizo zina nguvu ya kisheria, na hazihitaji kuidhinishwa na mwengine. Lakini hiyo haimaanishi kuwa rais anaweza kufanya chochote tu apendacho. Mahakama inaweza kuigeuza amri hiyo, au Congress inaweza kutunga sharia ya kuipinga. Zaidi ya hapo, rais ajaye anaweza kuitenguwa tu.
Kuna jengine. Rais wa Marekani anaweza kulikiuka bunge, mathalani, kwa kuingia kwenye makubaliano na serikali za nchi nyengine, ambako kawaida huwa lazima kuidhinishwe na thuluthi mbili ya wajumbe wa Seneti. Lakini anaweza badala yake kutowa "makubaliano ya kirais” ambayo hayahitaji ithibati ya bunge. Na makubaliano hayo huwa sahihi ikiwa tu Congress haikuyapinga au kutunga sharia ya kuyatangaza hayafai.
Kisha kuna suala la vikosi vya kijeshi. Licha ya kuwa rais wa Marekani ndiye kamanda mkuu wa majeshi yote, lakini ni bunge ndilo lenye madaraka ya kutangaza vita. Rais anaweza kutuma vikosi vya kijeshi kwenye mapigano bila ya idhini ya Congress, lakini hilo lina utata. Kwa mfano, Congress iliona kujihusisha kwa Marekani kwenye Vita vya Vietnam kulikuwa kumekwenda mbali sana na ikaingilia kati kwa kuweka sheria. Kwa ufupi, rais anayo madaraka fulani kwenye hili, hadi pale bunge linapoyatwaa.
Mwisho kabisa, ni suala endapo ni nani mwenye madaraka ya juu kabisa nchini Marekani, baina ya rais na vyombo vya kutunga sheria. Ikiwa raia ametumia vibaya madaraka yake au amefanya tendo la kihalifu, Baraza la Wawakilishi linaweza kuanza mchakato wa kumuondoa madarakani. Hii imetokea mara tatu ndani ya historia ya Marekani, lakini hakuna rais aliyetiwa hatiani. Badala yake, Congress inaweza kuyafanya maisha ya rais kama huyo kuwa magumu kwa kumkatia bajeti ya shughuli za serikali yake, lakini hilo nalo huenda lisiwafurahishe raia.
Mwandishi: Mohammed Khelef