1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden awania kulifunga gereza la Guantanamo Bay

Zainab Aziz Mhariri: Buwayhid, Yusra
13 Februari 2021

Rais wa Marekani Joe Biden anataka kulifunga gereza la Guantanamo Bay linalotumiwa kuwashikilia washukiwa wa ugaidi. Biden antaka kulifunga gereza hilo kabla ya muhula wake kumalizika.

https://p.dw.com/p/3pJjT
Guantanamo Häftling
Picha: picture-alliance/dpa/R. Schmidt

Hatua hiyo ya rais Biden ni katika muendelezo wa kuitimiza ahadi ya utawala wa Barack Obama ya kuifunga jela hiyo yenye utata. Obama mnamo mwaka 2016 alisema kuiendesha mahabusu hiyo haikuwa tu ni sera mbaya bali pia ni njia mojawapo ya kupoteza pesa, kwa sababu inagharimu zaidi ya dola milioni 445 kwa mwaka.

Wasaidizi wa Rais Joe Biden wameanza kulingalia upya swala la owepo wa jela hiyo ya Guantanamo Bay na wameanzisha majadiliano ya ndani yanayozingatia hatua ya kiutendaji itakayosainiwa na rais Biden katika wiki au miezi ijayo. Hayo yanaashiria juhudi mpya za kuondoa kile watetezi wa haki za binadamu wanachokiita kuwa ni jambo linaloitia doa Marekani kwenye sura ya ulimwengu.

Alipoulizwa katika mkutano na waandishi wa habari juu ya uwezekano wa kufungwa kwa gereza hilo lililopo nchini Cuba msemaji wa ikulu Jen Psaki amesema ni kweli hilo ni lengo na nia ya utawala wa rais Joe Biden.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Michael Reynolds/UPI Photo/imago images

Psaki amesema ameeleza kuwa serikali ya sasa ya Marekani kupitia idara ya usalama wa taifa inatathmini hali ya mambo ambayo utawala wa Biden umerithi kutoka kwa utawala uliopita.

Katika kampeni yake ya urais ya mwaka 2016, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alionyesha nia ya kuendelea kuwepo gereza la Guantanamo na kama alivyosema mwenyewe kwamba pangelikuwa ni mahala pa "kuwajaza watu wabaya."

Chama cha Republican kilitekeleza ahadi hiyo ya Trump mara tu kilipochaguliwa kuiongoza serikali licha ya baadhi ya wafungwa kuahidiwa kwamba wangeachiwa kutoka Guantanamo chini ya mtangulizi wake wa chama cha Democratic Barack Obama ambaye hakuweza kutimiza hatua hiyo kutokana na kutopata uungwaji mkono bungeni. Biden wakati huo alikuwa makamu wa rais wa Obama.

Gereza hilo la kijeshi lina wafungwa wanaohusishwa na kile kinachoitwa na Marekani "vita dhidi ya ugaidi", akiwemo Khaled Sheikh Mohammed wa Pakistan, ambaye alitangaza kuwa ndiye mkuu wa mashambulizi ya Septemba 11, mwaka 2001.

Baadhi ya mahabusu waliopo kwenye gereza la Guantanamo Bay
Baadhi ya mahabusu waliopo kwenye gereza la Guantanamo BayPicha: Getty Images/J. Moore

Hadi sasa gereza hilo bado lina wafungwa karibu 40 hadi 26 miongoni mwao wanaochukuliwa kuwa ni hatari iwapo wataachiwa huru huku kesi zao zikiendelea kusasua kutokana  na ugumu wa kesi hizo kisheria. Chini ya utawala wa Barack Obama, mahabusu wapatao 197 waliondolewa kwenye gereza la Guantanamo Bay na kupelekwa kwenye nchi nyingine.

Baada ya mashambulio ya tarehe 9/11, Jeshi la Marekani, chini ya rais George W. Bush, lilianzisha haraka kituo hicho cha kuwazuia watu kwenye eneo la ufukweni lililo chini ya Marekani mashariki ya Cuba, eneo hilo dogo lililokabidhiwa kwa Marekani na Cuba mnamo mwaka 1903, kama shukurani kwa taifa hilo jirani lenye nguvu kwa msaada wake kwa Cuba katika vita kati yake na Uhispania.

Vyanzo: AFP/AP