Rais wa Namibia ataka raia weusi wamiliki ardhi zaidi
1 Oktoba 2018"Kanuni ya mnunuzi wa hiari - muuzaji wa hiari haijatoa matokeo. Uzingatifu wa kina unapaswa kuelekezwa kwenye upokonyaji," alisema Rais Hage Geingob katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa kitaifa kuhusu ardhi katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek.
Taifa hilola kusini mwa Afrika linataka kuhamisha asilimia 43 ya hekta milioni 15 (maili 58,000 za mraba) za ardhi yake ya kilimo, kwa wakulima weusi ambao huko nyuma hawakupendelewa, ifikapo mwaka 2020. Mwishoni mwa 2015, asilimia 27 ya ardhi ilikuwa imegawanywa upya, kulingana na chama cha wakulima cha Namibia.
"Tunahitaji kupitia upya vipengele vya katiba vinavyoruhusu upokonyaji wa ardhi kwa kutoa fidia ya haki kuliko fidia inayostahili, na kutazama umiliki wa ardhi kwa wageni, hasa wamiliki wa ardhi wasiokuwepo," alisema Geingob.
Ni katika maslahi yetu sote, hasa wale walionacho, kuhakikisha tunapunguza pakubwa ukosefu wa usawa, kwa kuunga mkono ruwaza ya ugawaji upya inayohitajika ili kubadili muundo wa uchumi wetu. Tunapaswa wote kutambua ukweli kwamba huu ni uwezekezaji katika amani," alisema.
Jirani wa Namibia na chumi kubwa katika kanda hiyo, Afrika Kusini, pia iko katika mchakato wa kubadili sheria za umiliki wa ardhi - hatua ambayo imewatikisa wawekezaji wa ndani na nje, na kusababisha ujumbe wa utata wa twitter kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump mwezi Agosti akikosoa hatua zinazochukuliwa na serikali mjini Pretoria.
Kama ilivyo Afrika Kusini, maemfu ya Wanamibia weusi waliondolewa kwenye ardhi yao katika karne za 19 na 20, na kutupwa kwenye maeneo kame na wakati mwingine yaliosongamana maarufu kama 'Bantustans' huku wakinyimwa haki rasmi za umiliki.
Katika robo ya pili ya mwaka, uchumi wa Namibia ulinywea kwa robo ya tisa mfululizo, hiki kikiwa ndiyo kipindi kirefu zaidi tangu mwaka 2008.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef