1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Pakistan akataa kung'atuka madarakani

P.Martin11 Agosti 2008

Rais Pervez Musharraf wa Pakistan hatong'atuka madarakani - hayo ametamka msemaji wa Musharraf,huku serikali ya mseto ya nchi hiyo ikijiandaa kumshtaki mshirika mkuu wa Marekani,makosa ya kutumia vibaya madaraka yake.

https://p.dw.com/p/Euwi
President Pervez Musharraf of Pakistan meets reporters outside the White House after his meeting with United States President George W. Bush in the Oval Office ain Washington, D.C. on December 4, 2004. Musharraf said the two leaders believed that an independent Palestinian State was the key winning the war on terror. +++(c) dpa - Report+++
Rais wa Pakistan Pervez MusharrafPicha: dpa - Report

Siku ya Alkhamisi,serikali ya muungano inayoongozwa na chama cha waziri mkuu alieuawa Benazir Bhutto,ilitangaza kuwa itamshtaki Rais Pervez Musharraf kuwa ameitumbukiza nchi hiyo katika janga la kisiasa na uchumi wakati wa utawala wake wa takriban miaka tisa.Bunge linatazamia kufungua rasmi utaratibu wa kumshtaki Rais Pervez Musharraf baadae juma hili.Hata baadhi ya washirika wake wanamshinikiza jemadari huyo wa zamani ajiuzulu.

Lakini Rashid Qureshi alie msemaji wa Musharraf, amepuuza shinikizo hizo na kusema kuwa Rais Musharraf hatojiuzulu kwani hakuna sababu ya kumfanya kiongozi huyo kuondoka madarakani.Lakini alikataa kueleza zaidi kuhusu hatua zitakazochukuliwa na Musharraf.Wataalamu wanasema,miongoni mwa hatua anazoweza kuchukua ni kujaribu kulishinda bungeni azimio linalomtaka ajiuzulu au alivunje bunge hilo.Vile vile anaweza kutangaza hali ya hatari.

Hakuna rais aliewahi kushtakiwa nchini Pakistan,lakini wachambuzi wa kisiasa wanasema,safari hii yadhihirika kuwa utaratibu wa kumshtaki Musharraf hauwezi kuepukwa isipokuwa kama atajiuzulu.

Serikali ya muungano inajaribu kumpa Musharraf nafasi ya kujizulu bila ya kukabiliana na aibu ya kushtakiwa.Wakati huo huo inayashinikiza mabunge manne ya wilayani kupiga kura ya kumpinga Rais Musharraf.

Wabunge katika Wilaya ya Punjab yenye wakaazi wengi kabisa nchini Pakistan na iliyo ng'ome ya kiongozi wa serikali ya muungano Nawaz Sharif,hii leo walishangiria pendekezo la kupiga kura ya kutokuwa na imani na Musharraf.

Azimio hilo limesema Musharraf hafai kushika wadhifa wa urais kwa sababu ya hatia ya kukiuka Katiba ya nchi na kutumia vibaya madaraka yake na hivyo lazima ajiuzulu.Wabunge hao wakataja mapinduzi yaliyofanywa na Musharraf mwaka 1999 na hali ya hatari iliyotangazwa Novemba 2007.Wamesema,sera zake zimeitumbukiza Pakistan katika janga la kisiasa na uchumi.Mabunge mengine matatu yanatazamiwa kupiga kura baadae juma hili.

Kubakia Musharraf madarakani kutategemea sana iwapo jeshi litaendelea kumuonga mkono.Yeye alijiuzulu kama mkuu wa majeshi Novemba mwaka jana. Pakistan imetawaliwa na serikali za kijeshi kwa muda uliopindukia nusu ya historia yake ya miaka 61,lakini mrithi wa Musharraf,Jemadari Ashfaq Kayani ameeleza nia ya kutoliingiza jeshi katika masuala ya kisiasa.