Rais wa Palestina auomba Umoja wa Ulaya kuisaidia Palestina
23 Juni 2016Ingawa viongozi wa pande zote mbili wapo mjini Brussels hivi sasa, mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuwakutanisha pamoja umeshindikana. Na kwa sasa viongozi hao wamebaki wananyoosheana vidole vya lawama.
Ziara hiyo inakuja wakati kukiwa na jitihada za kimataifa za kutaka kufufua mazungumzo ya amani ya eneo la Mashariki ya Kati. Jaribio la mwisho liloongozwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry lilishindikana Aprili mwaka 2014. Tokea wakati huo hakujawahi kufanyika mkutano wowote wa ngazi ya juu kati ya maafisa wa Israel na wa Palestina.
Kulingana na taarifa zilizotolewa na ofisi ya Rivlin mjini Jerusalem zinasema rais huo yupo tayari kukutana na mwenzake wa Paleestina, lakini Abbas ndiye aliyakataa mpango huo wa kuwakutanisha wa Umoja wa Ulaya.
"Ninashangazwa na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas... mara kwa mara anakataa kukutana na viongozi wa Israel," amesema Rivlin. "Nilisikitishwa sana nilipopata habari kwamba amekataa kukutana. Hatutaweza kujenga imani kati yetu ikiwa hatutokutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana.
Wakati huo huo ofisi ya Abbas imetoa taarifa kwamba hakukuwa na mipango ya mkutano kati ya viongozi hao wawili.
Abbas azungumza mbele ya bunge la Umoja wa Ulaya
Abbas alielekea Brussels kuwasilisha maendeleo ya hivi karibuni kuhusu mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel.
Katika hotuba yake mbele ya bunge la Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Abbas aliuomba msaada umoja huwo kukomesha mpango wa Israel wa kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Halikadhalika ameiomba msaada wa kuanzisha mazungumzo ya amani ya kudumu.
"Nyinyi ni marafiki zetu, tusaidieni," Abbas aliwaambia wabunge wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, na kuongeza kuwa "Israel imeigeuza nchi yetu kuwa gereza la wazi."
Wabunge hawo walimpigia makofi na Abbas akauliza "Kwanini sheria ya kimataifa haitumiki katika suala hili la Israel?"
Umoja wa Ulaya umeahidi kutoa msaada wa kisiasa na kifedha kwa pande zote mbili iwapo watafikia makubaliano, huku kukiwa na shinikizo jipya la umoja huo la kusaidia kumaliza mgogoro huo wa muda mrefu.
Palestina ipo tayari kwa mazungumzo ya amani
Israel na Palestina hazikubaliani na jitihada za hivi karibuni zinazoongozwa na Ufaransa, za kutaka kufanyike mkutano wa amani ifikapo mwisho wa mwaka.
Abbas kwa upande wake amesema Palestina imeyakubali mapendekezo hayo ya Ufaransa, na inaishukuru kwa juhudi zake. Na ujumbe wake kwa Isarel amesema ni kwamba mikono ya Wapalestina ipo wazi, kukaribisha mazungumzo ya amani.
Lakini Israel imeukataa mpango huo wa Ufaransa, ikihofia jumuiya ya kimataifa huenda ikalazimisha suluhisho la mgogoro kati yao na Palestina.
Badala yake, Israel inasisistiza kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja baina ya nchi hizo mbili, bila ya masharti yoyote.
"Mazungumzo ya ana kwa ana ndiyo njia pekee ya kujenga imani, na kurejesha mazingira yatakayoleta amani," amesema Rivlin akiwa katika mkutano na waandishi habari pamoja na Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker na mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Federica Mogherini.
Mwandishi: Yusra Buwayhiddpae/ape
Mhariri:Yusuf Saumu