Rais wa Palestina Mahmud Abbas
6 Novemba 2009►
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina ,Mahmud Abbas, ameutosa utaratibu wa amani ya Mashariki ya Kati katika hali isiojulikana alipotangaza jana hadjharani kwamba, hatagombea tena awamu nyengine ya urais na hivyo, amefungua mlango wa kinyan'ganyiro cha madaraka kinachoweza kunufaisha chama hasimu HAMAS .
Wakati Israel imeitikia tangazo hilo kimya kimya,Marekani, yanaonesha imesharidhia kuondoka kwa Mahmud Abbas ingawa itakua tayari kushirikiananae katika wadhifa mwengine wowote.
ABBAS KUTOGOMBEATENA:
Rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya wapalestina,Mahmud Abbas, alisema uamuzi wake umechangiwa na kuzorota kwa juhudi za amani na Israel.Matamshi yake aliotoa kwa njia ya TV jana usiku yamezusha uvumi kwamba, hakutoa kauli ya mwisho na yamkini, ikawa ni mbinu tu kuihimiza Israel na mshirika wake Marekani kuwaridhia zaidi wapalestina wanayotaka. Abbas,ameelezea ni yake ya kutogombea tena uchaguzi uliopangwa Januari, mwakani na ambao unaweza lakini, kuahirishwa na hivyo, kurefusha kipindi chake cha sasa kwa muda usiojulikana.
JIBU LA ISRAEL:
Israel leo, imenyamaa kimya juu ya uamuzi wa bw.Abbas,lakini maafisa wa Israel, wamenon`gona kuwa, wangependa kumuona Bw.Abbas anaendelea madarakani.Gazeti la mrengo wa shoto la Israel "HAARETZ", limearifu kwamba,rais Shimon Peres wa Israel, alimpigia simu rais wa Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina ,siku moja kabla kutoa tangazo lake hilo ili kumshawishi asiondoke.
"Ukiondoka, wapalestina watapoteza fursa yao ya kujipatia dola huru....Hali ya mambo katika eneo hili itachafuka zaidi."-gazeti lilimnukulu rais Perez kumwambia Abbas.
Nae mjumbe wa wapalestina katika mazungumzo ya amani Saeb Erikat ,akitafsiri hatua aliochukua rais Mahmud Abbas alisema,
"Sio suali la urais, bali hii inatokana na serikali ya Israel kuendelea na ujenzi wa maskani za walowezi wa kiyahudi,kujiamulia kabisa mambo na kuamrisha nini la kufanywa.Na hata miaka 19 tangu kujaribu kusaka suluhisho la dola 2 ,yamkini rais amefadhahika na kuutambua ukweli wa mambo ulivyo."
MSIMAMO WA MAREKANI:
Taarifa kutoka Washington, Marekani, zinasema waziri wa nje bibi Hillary Clinton, alietembelea hivi punde Mashariki ya Kati adhihirika kuridhia hatua alioitangaza Bw.Abbas kutogombea uchaguzi hapo Januari.Alisema kuwa, atakuwa tayari kufanya kazi nae katika wadhifa wowote ule mpya atakaochukua.
ARAB LEAGUE:
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) Amr Mussa,amemtaka Bw.Mahmud Abbas, kuufikiria tena uamuzi wake wa kun'gatuka .
Viongozi wa Palestina wamesema kuwa, uamuzi wa Bw.Abbas kutogombea uchaguzi hapo Januari,mwakani, unatokana na kuvunjika kwake moyo na juhudi za Marekani kuzuwia ujenzi wa maskani za wayahudi -hatua ambayo wanataka ichukuliwe kwanza kabla kuanza tena mazungumzo ya amani.
Mwandishi: Ramadhan Ali/ APE/AFPE
Uhariri: Aboubakary Liongo