1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sri Lanka yafanya mabadiliko katika vikosi vya usalama

Yusra Buwayhid
25 Aprili 2019

Rais wa Sri Lanka Maithripala Sirisena amefanya mabadiliko katika vikosi vya usalama kwa kushindwa kuchukua hatua licha ya kupokea taarifa za onyo la mashambulizi ya kipindi cha Pasaka yaliyosababisha vifo zaidi ya 350.

https://p.dw.com/p/3HNnR
Sri Lanka Terroranschlag in Colombo | Sicherheitsmaßnahmen
Picha: Getty Images/A. Loke

Rais wa Sri Lanka amefanya uamuzi huo baada ya maafisa kushindwa kuchukua hatua licha ya kupokea taarifa za onyo la uwezekano wa kutokea mashambulizi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 350 wakati wa kipindi cha Pasaka.

Duru tatu tofauti zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba maafisa wa upelelzi wa Sri Lanka walionywa na India saa kadhaa kabla ya kutokea mashambulizo hayo. Lakini haijulikani wazi iwapo maafisa hao walichukua hatua yoyote kufuatia onyo hilo.

Katika hotuba ya televisheni kwa taifa usiku wa Jumanne, Rais Sirisena alisema atambadilisha mkuu wa vikosi vya majeshi katika kipindi cha masaa 24, na Jumatano aliwataka katibu wa ulinzi na mkuu wa jeshi la polisi kujiuzulu.

Bado hakutaja nani atakayechukua nafasi zao. Sirisena amesema alifichwa taarifa hizo za uwezekano wa kutokea mashambulizi na ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya maafisa wote walioshindwa kumuarifu mapema.

Sri Lanka Terroranschlag Trauer Ostern
Mama akiomboleza kifo cha mwanawe Shaini, 13, aliyefariki katika mashambulizi ya Sri LankaPicha: Reuters/A. Perawongmetha

"Kuna mjadala unaendelewa na watu wanaulizana kwanini vikosi vya usalama vya nchi hii havikuchukua hatua yoyote baada ya kupata taarifa za onyo kutoka nchi jirani. Lazima niseme kwamba mimi sikuarifiwa kuhusu onyo hilo na maafisa husika. Ningeliarifiwa, basi ingewezekani kuchukua hatua za haraka," amesema Rais Maithripala Sirisena.

Upinzani wapiga kauli ya rais Sirisena

Upande wa upinzani hata hivyo unakana kauli ya rais Sirisena na kusema kwamba baraza la usalama, waziri mkuu na rais mwenyewe pamoja na baraza la mawaziri wote walikuwa wanazo taarifa hizo hata kabla ya mashambulizi hayo kutokea. Mmoja wa wanasiasa wa upinzani Keheliya Rambukwella amesema katika mkutano na waandishi habari kwamba serikali kukaa kimya ulikuwa ni uamuzi wa kisiasa.

"Nadhani ulikuwa ni uamuzi wa kisiasa, walihisi hawapaswi kuwatikisa hawa viongozi wa Kiislam kwasababu ya kuogopa kukosa kura za waumini wao, na wananchi ndiyo walioumia, pamoja na takriban wageni 40," amesema Keheliya Rambukwella.

Polisi wa Sri Lanka wamesema wamewakamata watu wengine 18 wanaowashuku kuhusika na mashambulizi hayo ya Jumapili ya Pasaka, huku idadi ya vifo ikiwa imeongezeka na kufika watu 359.

Kundi linalojiita Dola la Kiislam IS limekiri kuhusika, baada ya maafisa wa Sri Lanka kusema waliojitoa muhanga kwa kujilipua walilipiza kisasi cha mashambulizi ya misikiti miwili ya New Zealand ya mwezi Machi yaliosababisha vifo 50.

Chanzo/rtre,ap