Kiir kusaini muafaka wa kugawana madaraka na waasi
26 Agosti 2015Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, ambaye alisimamia mazungumzo yaliyodumu miezi kadhaa yaliyolenga kumaliza vita hivyo vilivyodumu miezi 20 na kuwauwa maelfu ya watu, aliwasili mjini Juba kushuhudia hafla hiyo ya kusainiwa makubaliano baadaye leo.
Desalegn ataungana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Rais wa Sudan Omar al-Bashir na Yoweri Museveni wa Uganda, ambaye aliyatuma majeshi yake nchini Sudan Kusini kumuunga mkono Kiir wakati wa vita hivyo.
Msemaji wa Rais wa Sudan Kusini Ateny Wek Ateny amesema Kiir “atasaini makubaliano hayo ya amani”, lakini serikali imesema bado haijaridhishwa na baadhi ya yaliyomo kwenye mkataba huo wa kugawana madaraka. Karibu mikataba 7 ya kusitisha mapigano ilisainiwa na kisha kuvunjwa baada ya siku chache tu na mingine baada ya saa kadhaa, katika taifa hilo changa kabisa duniani ambalo lilijitenga kutoka kwa Sudan mwaka wa 2011.
Muafaka utakaosainiwa leo utawapa waasi wadhifa wa makamu wa rais, maana kuwa kiongozi wa waasi Riek Machar huenda akarejea katika nafasi hiyo ambayo alifukuzwa Julai 2013, miezi sita kabla ya vita kuanza. Machar tayari alisaini makubaliano hayo Agosti 17 mjini Addis Ababa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana liliongeza mbinyo kwa Kiir kusaini likionya kuwa liko tayari “kuchukua hatua ya haraka” ikiwa hatofanya hivyo. Hayo ni kwa mujibu wa rais wa sasa wa Baraza hilo Balozi wa Nigeria Joy Ogwu. Umoja wa Afrika leo umeonya kuwa makubaliano yoyote yatakayosainiwa ni sharti yatekelezwe, na ukatoa wito kwa pande zote mbili “kuhakikisha kuwa zinaleta maridhiano” na “kuyaweka mbele maslahi ya Sudan Kusini na watu wake na siyo yao binafsi”.
Ripoti ya jopo la watalaamu wa Umoja wa Mataifa, iliyotolewa jana, imesema pande zote katika mgogoro wa Sudan Kusini baina ya majeshi ya serikali na waasi zimewalenga raia. Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brian amesema “kiwango na ukatili wa machafuko hayo” tangu Aprili umekuwa mbaya kabisa.
Jopo hilo linalochunguza vikwazo vya Umoja wa Mataifa, limesema kampuni kuu ya silaha inayomilikiwa na serikali ya China iliuza silaha za zaidi ya dola milioni 20 kwa serikali ya Sudan Kusini mwaka jana, miezi kadhaa baada ya mgogoro kuanza.
Kampuni hiyo ya China North Industries Corp au Norinco, iliuza zana kama vile mitambo ya kufyatua makombora dhidi ya vifaru, makombora 1,200, karibu mitambo 2,400 ya kurusha maguruneti na aina tofauti ya risasi milioni 24. Ripoti hiyo pia imesema kuwa jeshi la Sudan Kusini ilinunua helikopta nne za mashambulizi tangu mwanzo wa mzozo huo. Nchi hiyo haikuwa na helikopta yoyote kabla ya hapo.
Mwandishi: Bruce Amani/AP/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel