1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Tanzania aamuru kukamatwa wasimamizi wa MV Nyerere

22 Septemba 2018

Rais wa Tanzania John Magufuli asema waendeshaji na wasimamizi wa kivuko MV Nyerere kilichozama kwenye Ziwa Victoria wakamatwe huku uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hilyo ukiendelea.

https://p.dw.com/p/35KBS
Tansania Fährunglück auf dem Victoriasee
Picha: DW/M. Magessa

Miili ya takriban watu 136 imeshapatikana kufuatia ajali ya kuzama kivuko MV Nyerere katika Ziwa Victoria nchini Tanzania. Rais John Pombe Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo na kuagiza bendera ya nchi hiyo ipepee nusu mlingoti. 

Magufuli ameelezea wasiwasi wake kwamba idadi ya watu waliokufa huenda ikaongezeka alipozungumza na waandhishi wa habari. Ameeleza kuwa rasmi kivuko hicho cha MV Nyerere kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 101, lakini kulingana na takwimu zinazojumuisha miili iliyopatikana hadi sasa pamoja na manusura, ni wazi kwamba chombo hicho kilikuwa kimebeba abiria kupita kiasi.

Rais Magufuli alifahamisha pia kwamba nahodha wa MV Nyerere amekamatwa na inaaminika kuwa hakuwamo ndani ya kivuko hicho wakati ajali ilipotokea na wakati huo huo ameamuru kukamatwa kwa wote waliohusika na ajali hiyo, ili waweze kuhojiwa huku uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo ukiendelea.

Viongozi mbalimbali ulimwenguni wanaendelea kutuma salamu za rambirambi. Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amesema amehuzunishwa sana na ajali hiyo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na kansela wa Ujerumani Angela Merkel ni miongoni mwa viongozi waliotuma salamu za rambirambi kwa jamaa za wahanga wa ajali hiyo, serikali pamoja na wananchi wa Tanzania kwa jumla.

Rais wa Tanzania John Magufuli
Rais wa Tanzania John MagufuliPicha: Imago/Xinhua Afrika

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amemtumia salamu za rambirambi rais wa Tanzania John Magufuli na kuelezea huzuni yake kwa niaba ya wananchi wa Kenya kutokana na ajali iliyotokea katika nchi jirani ambapo amesema moyo wake uko pamoja na Watanzania walioondokewa na ndugu zao baada ya ajali hiyo mbaya kutokea.

Kivuko MV Nyerere, kilizama mnamo siku ya Alhamisi alasiri. Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amesema makadirio ya awali yalionyesha kwamba kivuko hicho kilikuwa na zaidi ya watu 300 waliokuwa wanasafiri kutoka Bugolora kwenda Kisiwa cha Ukara, lakini idadi halisi ya abiria waliokuwa kwenye chombo hicho bado haijulikani. Bwana Mongella amesema shughuli ya kuitambua miili ya watu waliozama kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere ilianza hapo Ijumaa jioni.

Kulingana na wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA, wanaosimamia huduma za feri nchini Tanzania, chombo hicho kilizama mita kadhaa kutoka kwenye gati iliyo karibu na kisiwa cha Ukara katika wilaya ya Ukerewe.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/DPAE

Mhariri: Yusra Buwayhid