Rais wa UEFA aitaja tabia ya Rubiales kama "isiyofaa"
31 Agosti 2023Rais wa UEFA Aleksander Ceferin ameliambia gazeti la Ufaransa la L'Equipe kuwa, alichokifanya Rubiales sio sahihi japo uchunguzi wa kinidhamu wa FIFA utaamua juu ya hatua itakayochukua.
"Kesi yake iko mikononi mwa bodi ya nidhamu ya FIFA. Maoni yoyote nitakayoyatoa juu ya tukio hilo huenda yakatafsiriwa kama kuongeza shinikizo," Ceferin ameeleza.
Soma pia: Shirikisho la kandanda Uhispania lamtaka Rubiales ajiuzulu
Mnamo siku ya Jumamosi, shirikisho la soka duniani FIFA lilimzuia Rubiales kujihusisha na masuala yote yanayohusu soka kwa muda wa miezi mitatu wakati FIFA ikichunguza madai kuwa alimbusu mchezaji wa timu ya taifa ya Uhispania ya wanawake Jenni Hermoso bila ridhaa yake baada ya Uhispania kushinda Kombe la Dunia.
Rubiales mwenye umri wa miaka 46 amesema atatumia uchunguzi huo wa FIFA kuonyesha kwamba hana hatia. Mkuu huyo wa shirikisho la soka la Uhispania amekuwa akijitetea kuwa, tukio la busu lilifanyika kwa ridhaa yake Hermoso.
Ceferin ameongeza kuwa anasikitishwa kwamba sakata hilo la busu limefunika ushindi wa Uhispania katika mashindano ya Kombe la Dunia la Wanawake.