PPRD nchini Kongo yaapuuzilia madai ya hifadhi kwa ADF
19 Julai 2023Katika mahojiano ya hivi karibuni na shirika la habari Reuters, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema kuwa, namnukuu: "Serikali ya Joseph Kabila, ikiungwa mkono na baadhi ya watendaji wa kikanda na kimataifa, iliwapa ADF kukodisha bila malipo katika Kivu Kaskazini na Ituri. Walikuwa wakichimba dhahabu, wakiuza mbao, wakivuna kakao za watu, wakitoza kodi..." Mwisho wa kumnukuu.
Madai ya Museveni chakikasirisha chama cha PPRD
Ila madai haya ya Rais Museveni yamekikasirisha chama cha PPRD cha rais wa zamani Joseph Kabila. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, chama cha PPRD kimekanusha madai yote ya Rais Museveni, kikisema ni uongo kwa lengo la kuyumbisha usalama tena mashariki mwa DRC. Chama hiki kinasema Ujumbe huu unaonyesha hofu ya serikali ya Félix Tshisekedi ambayo inawapa faida za kuyumbisha usalama Mashariki. Ferdinand Kambere ni katibu wa chama cha PPRD akiwa mjini Kinshasa.
PPRD yadai Uganda yashirikiana na Rwanda kuyumbisha usalama wa Kongo
Chama cha PPRD ambacho kimesusia uchaguzi unaoandaliwa mnamo desemba mwaka huu kinatoa angalisho kwa Uganda kikibaini kwamba inashirikiana na Rwanda kuyumbisha usalama wa Kongo. Upande wa chama tawala cha UDPS chake Rais Tshisekedi, baadhi ya wanachama wanaonya PPRD kubaki kimya wakishotea utawala wa Kabila kuchangia pakubwa katika vita vilivyosababisha mauaji, ubakaji na maafa makubwa mashariki nchini Kongo tangu zaidi ya miaka ishirini na tano. Elie Mugisho ni msemaji wa chama cha UDPS mtaani Ibanda akiwa mjini Bukavu
Kundi la ADF lilikuwa likiendesha mashambulizi katika eneo la Ruwenzori
Kundi la ADF lililoanzishwa mwaka 1996 lilikuwa kundi la waasi wa Uganda ambalo liliendesha mashambulizi katika eneo la Ruwenzori magharibi mwa Uganda. Hatimaye waasi hao walivuka mpaka kukimbilia katika misitu ya mashariki mwa Kongo, ambako wameendesha shughuli zao tangu wakati huo.