Rais Putin akutana na Assad
18 Mei 2018Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Kremlin, akizingatia mafanikio makubwa ya Jeshi la Syria, Putin alimuarifu al-Assad kwamba hali ni muwafaka kuweza kuimarisha mchakato wa kisiasa na kwamba huenda majeshi ya kigeni yakaanza kuondoka nchini Syria.
Kiongozi wa Syria aliwahi kusema hivi karibuni kwamba mafanikio upande wa kijeshi yanamaanisha kwamba serikali yake inafanikiwa katika kurejesha hali ya kawaida inayofungua njia kwa raia wengi wa nchi hiyo kurudi kwenye makaazi yao.
Uundwaji wa kamati ya kikatiba ya Syria
Pamoja na hayo alinukuliwa akisema yeye na Putin walizungumzia juu ya kamati ya kikatiba inayokusudiwa kuundwa, ili kuzungumzia marekebisho ya katika katiba , kufuatia mkutano wa Baraza kuu la majadiliano la Syria uliofanyika mjini Sochi mwezi Januari.
Wanasiasa wakuu wa upinzani waliyasusia mazungumzo hayo, lakini Assad amesema Syria iko tayari kuanza kufanya kazi na Umoja wa Mataifa, kuandaa muswaada wa marekebisho ya katiba. Urusi ni mshirika mkubwa wa Bashar al-Assad na msada wa kijeshi kutoka Moscow umemsaidia rais huyo wa Syria kupata mafanikio makubwa kuyakomboa maeneo yaliokuwa yakidhibitiwa na wapinzani wake katika vita mnamo miezi ya hivi karibuni, yakiwemo yale yanayouzunguka mji mkuu Damascus.
Rais Putin asema magaidi waweka chini silaha
Katika matamshi yake yaliochapishwa hapo kabla katika mtandao wa Ikulu, Rais Putin alisema magaidi wameweka chini silaha katika maeneo muhimu nchini Syria, jambo ambalo limefanikisha kurirejesha miundo mbinu katika hali ya kawaida na hasa kumaliza harakati zao za kijeshi karibu na mji mkuu Damascus. Kwa upande wake al-Assad aliwashukuru wanajeshi wa Urusi na hasa wale wa kikosi cha anga, kwa mchango wao muhimu, aliouita " wa kupambana na magaidi."
Urusi ni miongoni mwa nchi tatu pamoja na Uturuki na Iran zinazojiona kuwa na usemi katika mazungumzo kati ya upinzani nchini Syria na serikali, chini ya kile kinachoitwa mchakato wa Astana. Mazungumzo kati ya pande hizo yamekuwa yakiendelea kila wakati katika mji mkuu huo wa Kazakhstan tangu 2017, kwa lengo la kukamilisha mchakato wa amani unaoongozwa na Umoja wa mataifa.
Mazungumzo ya Putin na Assad mjini Sochi jana yamekuja siku moja kabla ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kukutana na Rais Putin mjini humo, huku Syria ikiwa ni moja wapo ya masuala katika ajenda ya mazungumzo. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amesema haamini kuwa Urusi itamuunga mkono al-assad kwa muda mrefu zaidi. Akaongeza ," Mustakbali wa muda mrefu na mchinjaji al-Assad, ambaye ana damu mikononi mwake si jambo litakalotokea." Zaidi ya Wasyria 400,000 wamekufa katika mzozo huo ulioanza 2011 kwa maandamano yakudai mageuzi nchini humo. Mamilioni wengine wamekimbilia nchi za nje au kuwa wakimbizi wa ndani.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpa
Mhariri: Grace Patricia Kabogo