Rais wa Uturuki Erdogan ziarani Afrika
2 Juni 2016Ni ujumbe mkubwa, ambao rais Recep Tayyip Erdogan anaongozana nao katika ziara hiyo. Wawakilishi zaidi ya mia moja wa masuala ya kiuchumi , wamo katika ujumbe wake , ili kuweza kugusa kila sekta ya kiuchumi katika nchi hizo za Kenya na Uganda.
Mkutano kati ya Erdogan na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni ni wa kihistoria. Hii ni ziara ya kwanza rasmi ya rais wa Uturuki nchini Uganda. Kwa jumla ziara hii inatoa kwa Uturuki hali ya kujiamini zaidi, kama ilivyoelezwa katika taarifa katika mtandao wa interneti kwamba ziara ya rais katika bara la Afrika imeanza.
Harakati hizi za Uturuki katika bara la Afrika sio mpya, anasema Christian Johannes Henrich, mkuu wa kituo cha utafiti wa masuala ya utawala wa himaya katika Ulaya ya kusini na eneo la Kaukasus, alipozungumza na DW.
"Tangu mwaka 1998, miaka minne kabla ya kuingia madarakani Erdogan na chama chake cha AKP, msogeleano ulianza na waziri mkuu Mesut Yilmaz. Wakati huo Uturuki ilikuwa tayari na ajenda kuhusu Afrika, lakini kutokana na matatizo ya ndani haikuweza kutekelezwa. Waligundua Waturuki kwamba katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ndiko kwenye ukuaji wa uchumi."
Uchumi barani Afrika
Mawazo haya yalimgusa Erdogan , lakini kwa njia tofauti na mtangulizi wake. chini ya utawala wa Erdogan msisitizo zaidi ni juu ya masuala ya kiuchumi. Anataka kujihusisha zaidi na nchi za Afrika zenye Waislamu wa madhehebu ya Sunni, ama sehemu ya wakaazi wa nchi hizo.
Uganda na Kenya, nchi hizi zina umuhimu mkubwa zikiwa na kiwango kikubwa cha Waislamu wa madhehebu ya Sunni, anasisitiza Christian Johannes Henrich.
Kwa kuwa na sera imara za mambo ya kigeni katika bara la Afrika, Uturuki inataka kujihakikishia kuwa na udhibiti wa kimkoa katika kiwango cha kimataifa. Katika bara la Afrika , Uturuki inaingia katika ushindani na mataifa mengine kama Brazil, India na China.
Na inaingia si kwa kuwania mali ghafi za bara la Afrika lakini kutaka uungwaji mkono katika Umoja wa Mataifa, anasema Christian Johannes Henrich. Erdogan na serikali yake inayoongozwa na chama chake cha AKP anajihusisha na kuchukua jukumu la juu katika siasa za dunia, siasa ambazo zinatafsiriwa kuwa za himaya ya Osmani mambo leo.
"Nina wasi wasi kwamba Uturuki si tu inataka kurejesha maeneo yake ya wakati wa himaya ya Osman, lakini hivi sasa inataka pia kujipanua hadi Afrika. Nafikiri Uturuki inataka kujiweka katika kila kanda."
Mchoraji wa vikatuni nchini Kenya Gado, ametayarisha mchoro kwa ajili ya DW unaomuonesha Erdogan akiwa na kilemba akiwasili katika bara la Afrika kama kiongozi wa himaya ya Osman mamboleo, akileta zawadi za kukamatwa kwa waandishi habari, wapinzani na ndugu wanaharakati wa vyama vya kijamii.
Mwandishi: Antonio Cascais / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Hamidou Ommilkheir