Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma afukuzwa ANC
29 Julai 2024Vyombo kadhaa vya habari nchini Afrika kusini vimeripoti kwamba,kamati ya nidhamu ya chama tawala cha African National Congress ANC imepitisha maamuzi ya kumtimua chamani aliyekuwa rais wa taifa hilo Jacob Zuma.
Inaelezwa kwamba hatua hiyo imetokana na Zuma kukiongoza chama hasimu katika uchaguzi uliopita wa mwezi Mei.
Vyombo vya habari vimeripoti taarifa hiyo kwa kunukuu waraka uliovuja.
Soma pia: Ramaphosa atangaza baraza jipya la mawaziri
Uamuzi huo ambao bado haujatangazwa rasmi ulichukuliwa baada ya kufanyika mchakato wa kamati ya nidhamu ya chama ulioanzishwa mwanzoni mwa mwezi huu dhidi ya kiongozi huyo wa zamani ambaye bado ana umaarufu nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa ufafanuzi ulioonekana na shirika la habari la AFP katika waraka huo, Zuma ana haki ya kukata rufaa kuupinga uamuzi wa kamati hiyo ndani ya kipindi cha siku 21.
Chama cha ANC kilimsimamisha chamani Zuma mwezi Januari na mwezi mmoja baadae mwanasiasa huyo akatangaza kukiunga mkono chama kipya cha uMkonto weSizwe.