1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Brazil Lula afungwa jela

13 Julai 2017

Rais wa zamani aliyeipatia Brazil umaarufu katika jukwaa la kimataifa amepatikana na hatia ya kupokea rushwa na utakatishaji fedha. Luiz Inacio Lula da Silva amepewa miaka tisa na nusu jela

https://p.dw.com/p/2gRKS
Brasilien Luiz Inacio Lula da Silva und Dilma Rousseff
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Peres

Hukumu hiyo ya kihistoria imedhihirisha kuwa hakuna anayeweza kukwepa mkono wa sheria katika uchunguzi mpana wa rushwa unaofanywa katika nchi hiyo ya Amerika Kusini

Hukumu dhidi ya Rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva ni ushindi unaomhusisha mtu wa ngazi ya juu kabisa katika uchunguzi huo wa rushwa, ambao tayari umewanasa wanasiasa na wafanyabiashara kadhaa maarufu. Zaidi ya dola bilioni 3 zilizopotea katika njia zisizo za kisheria zimerejeshwa.

Wakati Jaji Sergio Moro aliutetea uamuzi huo kuwa uliozingatia kikamilifu sheria, Silva alidai ni njama ya kisiasa na anatarajiwa kuwahakikishia wafuasi wake kuhusu mipango yake katika kikao cha habari baadaye leo.  Lula amehukumiwa kifungo cha karibu miaka kumi gerezani, na atabaki huru wakati kesi ya rufaa ikisikilizwa. Ni rais wa kwanza wa zamani kuhukumiwa mahakamani tangu demokrasia iliporejeshwa katika miaka ya 80 nchini humo.

Brasilien - Temers Reaktion auf den Senat
Rais wa sasa Michel Temer anakabiliwa na mbinyoPicha: Reuters/A. Machado

Wakati huo huo, rais wa sasa Michel Temer, anakabiliwa na kesi yake mwenyewe ya rushwa. Mchambuzi wa siasa katika chuo kikuu cha Fundacao Getulio Vargas mjini Rio de Janeiro Sergio Praca anasema sio kawaida kwa rais wa zamani kuhukumiwa kwa rushwa na wakati huo huo rais aliyeko madarakani pia akichunguzwa. Anasema ni siku muhimu katika historia ya Brazil, iwe ni kwa mazuri au kwa mabaya.

Wabrazil wameishi katika miaka mitatu ya misukosuko wakati uchunguzi huo mpana ukifichua kiwango cha rushwa ambacho kimewashtua wengi nchini humo. Rais Dilma Rouseff alivuliwa madaraka kupitia kura ya kutokuwa na imani naye kwa ubadhirifu wa bajeti ya serikali. Na sasa mrithi wake, Temer, anakabiliwa na mbinyo wakati bunge likiamua kama anapaswa kuachishwa kazi au kushitakiwa.

Silva, Kiongozi mkakamavu aliondoka madarakani mwishoni mwa 2010 akiwa na umaarufu mkubwa, baada ya kuyatumia mafanikio ya kiuchumi katika kufadhili mipango ya kijamii ambayo iliwaondoa katika umaskini  mamilioni ya Wabrazil na kutanua jukumu la kimataifa kwa taifa hilo kubwa kabisa la Amerika Kusini.

Brasilien Dilma Rouseff
Rais Dilma Rouseff alivuliwa madaraka Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Peres

Silva mwenye umri wa miaka 71, bado anaheshimika – kutokana na sera zake za kiuchumi na jukumu lake katika kupigania demokrasia wakati wa kipindi cha udikteta nchini humo. Anazingatiwa na wengi kuwa katika mstari wa mbele katika kugombea uchaguzi wa rais mwaka ujao.

Timu ya mawakili wa Silva ilitoa taarifa kali baada ya hukumu hiyo, ikiyaita mashitaka hayo kuwa shambulizi dhidi ya demokrasia na kuapa kuthibitisha kuwa rais huyo wa zamani hana hatia.

Silva alituhumiwa kwa kupokea jengo moja la ufukweni na kufanyiwa ukarabati jengo hilo kama malipo ya shukrani kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya OAS. Silva hakuwahi kumiliki jengo hilo, lakini waendesha mashitaka wanahoji ilikuwa ni kwa ajili yake. Silva pia anakabiliwa na mashitaka mengine manne. Anakanusha kufanya kosa lolote.

Kesi hiyo sasa inakwenda mbele ya kundi la mahakimu. Kama wataushikilia uamuzi huo, katiba ya Brazil inasema Silva atazuiuwa kugombea. Pamoja na hukumu ya Silva ya miaka tisa na nusu jela, pia mwanasiasa huyo amezuiwa kushikilia wadhifa wa umma kwa miaka 19. Ofisi ya mwendesha mashitaka iliyoshughulikia kesi hiyo imesema itakata rufaa hukumu hiyo ili kutaka iongezwe.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Daniel Gakuba