Rais wa zamani wa Misri Morsi afariki mahakamani
18 Juni 2019Rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia ambaye alipinduliwa na jeshi mnamo mwaka 2013 baada ya mwaka mmoja madarakani, Mohammed Morsi, alianguka mahakamani wakati kesi yake ilipokuwa ikisikilizwa na kufariki, televisheni ya taifa na familia yake ilisema.
Morsi aliyekuwa na umri wa miaka 67 alikuwa amemaliza kuihutubia mahakama, akizungumza akiwa katika chumba cha glasi alimowekwa wakati wa vikao vya kusikilizwa kesi yake na kuonya ana 'siri nyingi' ambazo angeweza kuzifichua, afisa wa idara ya mahakama alisema.
Dakika chache baadaye, Morsi alianguka na kupoteza fahamu ndani ya chumba hicho cha glasi, aliongeza kusema afisa huyo aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa sababu hakuwa na amri ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Katika kauli zake za mwisho, Morsi aliendelea kusisitiza alikuwa rais halali wa Misri, akidai mahakama maalumu, mmoja wa mawakili wake, Kamel Madour, aliliambia shirika la habari la Associated Press.
Televisheni ya taifa ilisema Morsi alikufa kabla hajapelekwa hospitali. Chama cha Morsi cha Udugu wa Kiislamu kimeilaumu serikali kwa kumuua kupitia mazingira mabaya gerezani. Katika taarifa kundi hilo limetaka uchunguzi wa kimataifa ufanywe kubaini chanzo cha kifo cha Morsi na kuwataka Wamisri waandamane nje ya balozi za Misri kote ulimwenguni.
Morsi, ambaye anafahamika kuugua kisukari, amekuwa gerezani tangu alipopinduliwa mwaka 2013, akitengwa na wafungwa wengine kwa kuwekwa katika chumba chake peke yake na kunyimwa haki ya kuwa na wageni. Familia yake iliruhusiwa kumtembelea mara tatu wakati wa kipindi hicho.
Mwendesha mashitaka mkuu wa Misri amesema mwili wa Morsi utafanyiwa uchunguzi kubaini sababu ya kifo chake.
(ape, afpe)