1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Zambia Levy Mwanawasa amefariki dunia.

Saumu Mwasimba19 Agosti 2008

Kiongozi huyo amefariki katika hospitali moja mjini Paris Ufaransa ,

https://p.dw.com/p/F154
Picha: AP

Rais Mwanawasa amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu kiharusi ambapo alikuwa amelazwa tangu mwishoni mwa mwezi Juni katika hospitali moja nchini Ufaransa.

Rais Mwanawasa alianza kupata umaarufu akiwa kiongozi wa chama cha Movement for Multiparty Democracy MMD kilichomaliza utawala wa chama kimoja wa Rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda 1991.

Wakati hali yake ya kisiasa ikionekana kama imemalizika Mwanawasa kwa mshangao wa wengi aliibuka tena alipoteuliwa na mtangulizi wake Rais Frederick Chiluba kuwa mrithi wake.

wachambuzi wanauona ni uamuzi ambao Bw Chiluba ataujutia, baada ya kujikuta akifikishwa mahakamani kwa mashitaka ya ubathirifu wa mamilioni ya dola -fedha za serikali, huku Mwanawasa akila kiapo kupambana na ufisadi.

Katika siasa za kanda ya kusini mwa Afrika, Mwanawasa ni kiongozi pekee wa eneo hilo aliyetokeza wazi kumkosoa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kuhusiana ana hali ya kisiasa nchini mwake, wakati wengine walibakia kimya. Mwanawasa akaifananisha hali ya kiuchumi ya Zimbabwe kuwa sawa na meli inayozama.

Nyumbani nchini Zambia utawala wake unasifika kwa kuweka sawa hazina ya akiba ya fedha za kigeni kufikia kiwango cha euro 700 milioni wakati kiwango cha ughali wa maisha kimeteremka hadi asili mia 10.

Pamoja na hayo aliungama kwamaba umasikini bado ni tatizo huku wengi miongoni mwa Wazambia bado wakiishi chini ya kiwango cha ufukara.

Jee kifo cha kiongozi huyo kimepokewaje na Wazmabia wenyewe.

Kiongozi huyo wa Zambia ana rekodi ya kuugua kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja kisukari na matatizo yaliotokana na ajali ya barabarani aliyoipata 1993 alipokua makamu wa rais .

Alijijengea sifa alipojiuzulu umakamu wa rais katika utawala wa Chiluba kupinga kukithiri kwa visa vya rushwa na biashara ya madawa ya kulevya miongoni mwa maafisa wa serikali wa ngazi ya juu.

Alichaguliwa Rais wa tatu wa zambia Januari 2002.

Baada ya kumuacha mkewe wa kwanza, Rais Mwanawasa alimuowa mawanashertia wenzake Maureen .Marehemu ameacha pia watoto sita.

►◄