Ramallah. Palestina na Israel huenda wakatia saini makubaliano.
29 Septemba 2007Rais wa Palestina Mahmud Abbas amesema kuwa Israel na mamlaka yake huenda wakatia saini makubaliano ya amani katika muda wa miezi sita ijayo baada ya mkutano wa kimataifa wa amani unaopangwa kufanyika mwezi Novemba. Mkutano huo unaodhaminiwa na Marekani unapaswa kuweka msingi wa utatuzi wa masuala juu ya hali ya mwisho ya maeneo ya mamlaka ya Palestina, amesema Abbas. Katika hotuba yake katika baraza kuu la umoja wa mataifa jana Ijumaa , Abbas ametoa wito kwa dunia kuchukua nafasi hii katika mkutano wa Novemba kufanyakazi kuelekea katika uundwaji wa taifa la Palestina. Kiongozi huyo wa mamlaka ya Palestina , ambaye amekutana na viongozi kadha muhimu wa kigeni wakati wa ziara yake mjini New York , amesema kuwa mazungumzo yataanza mjini Washington hapo Novemba 15.