1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RANGOON:Serikali ya Burma yatishia kuchukua hatua kali dhidi ya watawa

25 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBMr

Utawala wa kijeshi wa Myanmar zamani ikiitwa Burma umetishia kuchukua hatua dhidi ya watawa wa dini ya Budda ambao wanaongoza maandamano makubwa kabisa kuupinga utawala huo.

Waziri anayehusika na masuala ya dini Brigadier General Thura Myint Maung ametoa onyo kwa watawa hao kutovunja sheria na taratibu za dini yao, mnamo wakati ambapo mji mkuu Rangoon umeendelea kugubikwa na maandamano hayo.

Amewalaumu watawa hao kwa upinzani unaelekea kuhatarisha amani ya nchi hiyo.

Rais George Bush wa Marekani anatarajiwa kutangaza vikwazo vipya kwa utawala wa kijeshi wa Burma.

Mshauri wa masuala ya kiusalama wa Marekani Stephen Hadley amesema kuwa vikwazo hivyo vitakavyotangazwa na Rais Bush katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni pamoja na kuwazuia viongozi wa utawala huo kuingia nchini Marekani.

Watawa hao ni watu wanaoheshimiwa sana nchini Burma na kitendo chochote kitakachochukuliwa na utawala huo wa kijeshi kusambaratisha maandamano yao, kitazidisha upinzani zaidi.

Hata hivyo kuna hofu ya kwamba huenda utawala huo wa kijeshi unaweza kurejea tukio la mwaka 1988 wakati ulipowaua watu zaidi elfu tatu katika kuyazima maasi yaliyoibuka kutaka demokrasia.