1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RB Leipzig kuonja joto la Champions League

Sekione Kitojo
13 Septemba 2017

Swali kwamba je fedha zinaweza kuleta ushindi uwanjani? Limejibiwa na kikosi cha Paris Saint-Germain ya Ufaransa pale washambuliaji  wake walipopachika mabao dhidi  ya  Celtic Glasgow ya  Scotland.

https://p.dw.com/p/2jtwq
FIFA Confederations Cup 2013 | Neymar (picture-alliance/ZUMAPRESS)
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/M. Machado

Washambuliaji Neymar, Kylian  Mbappe  walionunuliwa  na  klabu  hiyo  kwa  kitita cha  juu  kabisa  pamoja na  Edson Cavani  kila  mmoja  alipachika mabao  mawili.

Messi  wa  Barcelona  na Robert  Lewandowski  wa  Bayern  Munich nao  pia  walionesha  umahiri  wao wa kupachika  mabao. Huo ulikuwa mwanzo  wa  msimu  mpya  wa  kinyang'anyiro  cha  kombe la  mabingwa  barani  Ulaya. Leo hii michuano  hiyo  inaendelea kwa michezo  mingine  minane.

Champions League - FC Barcelona vs Juventus
Wachezaji wa Barcelona wakimpongeza Messi(katikati) alipopachika bao dhidi ya CelticPicha: Reuters/S. Vera

RB Leipzig  inayodhaminiwa  na  kampuni  inayotengeneza  kinywaji cha  kuongeza  nguvu  mwilini Red Bull , inajitupa uwanjani jioni  ya leo ikijaribu kwa  mara  ya  kwanza kuangalia  hali  ya  hewa  katika anga  hizo  za  juu  katika  soka  la  Ulaya ikipambana  na  AS Monaco  ya  Ufaransa.

RB Leipzig  iko  tayari kwa  Champions League, lakini  Champions League  iko  tayari  kwa  Leipzig ?  Hilo  ni  swali  la  dola  milioni mbili.  Ikija  katika  kuorodhesha  timu  ambazo zinauwezo  wa kunyakuwa  kombe  hilo , kwa  kawaida  majina  makubwa  ndio hutajwa , lakini  hakuna mtu atakayeitaja  RB Leipzig  katika  orodha hiyo. Je  hilo  litakuwa  kosa  kubwa ? mashabiki  wa  Ulaya  na duniani  kwa  jumla  jioni  ya  leo watapata  fursa  ya  kuangalia  kwa karibu  kikosi kinachopewa  mafunzo  na kocha  raia  wa  Austria Ralph Hasenhuettl.

Bundesliga Hamburger SV - RB Leipzig
Kikosi cha vijana wa RB Leipzig ya UjerumaniPicha: picture-alliance/CITYPRESS 24/M. Taeger

Borussia  Dortmund

Borussia  Dortmund inaingia  uwanja  wa  Wembley  leo  jioni ikiwa na  kumbukumbu  ya  kutoka  patupu katika  fainali  ya  Champions League  mwaka  2013  dhidi  ya  Bayern Munich , licha  ya  kwamba mara  hii  inacheza  na  timu  kutoka  Uingereza Tottenham Hot Spurs na  sio  katika  fainali  bali  ni  mchezo  wa  kwanza  wa  kundi H. Mchezo  mwingine  wa  kundi  H unazikutanisha   Real Madrid ambao  ni  wenyeji  wa  pambano  lao  dhidi  ya  APOEL Nicosia  ya Cyprus.

Liverpool   ya  Uingereza  nayo  imerejea  katika  kinyang'anyiro hicho  na  kocha  Juergen Klopp  anahaja  ya  kuonesha  kwamba kufika  fainali  mwaka  2013 akiwa  na  Borussia  Dortmund ya Ujerumani  haikuwa  jambo  la  kubahatisha.Liverpool inaonshana kazi  na  Seville  ya  Uhispania.

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Hertha BSC 2:0 Mario Götze
Wachezaji wa Borussia Dortmund wakishangiria bao Picha: picture-alliance/SvenSimon/J. Kuppert

Kocha  mwenye  mafanikio  makubwa  katika  soka  barani  Ulaya Pep Guardiola  anajaribu  mitambo  yake  tena  mara  hii  akiwa  na Manchester  City akikabiliwa  na  Fayenoord  ya  Uholanzi. Napoli ya  Italia  itakuwa  nchini  Ukraine  ikiumana  na  Shakhtar Doneszk. Porto  ya  Ureno ina  miadi  na  Besiktas  ya  Uturuki  na  Maribor  ya Slovenia  inapambana  na  Spartak Moscow  ya  Urusi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Idd Ssessanga