1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RB Leipzig wawararua Freiburg

28 Agosti 2017

Mshambuliaji wa Ujerumani Timo Werner, alifunga mabao mawili wakati RB Leipzig ilitoka nyuma na kuwazaba Freiburg 4-1 na kuurejesha msimu wao wa Bundesliga katika mkondo sahihi

https://p.dw.com/p/2izB0
Bundesliga RB Leipzig - SC Freiburg Jubel
Picha: picture-alliance/dpa/S. Kahnert

Leipzig iliyafunga mabao manne bila jibu katika kipindi cha pili, baada ya kufungwa goli moja katika kipindi kibovu cha kwanza. Ni matokeo ambayo kocha Ralph Hassenhutl amesema yalihitajika hasa ikizingatiwa kuwa mechi ya kwanza walizabwa mbili moja na Schalke

Katika mechi nyingine ya jana, Hanover ilipata ushindi katika kipindi cha pili kwa kuifunga Schalke 1-0 bao lililofungwa na mshambuliaji wa Brazil Jonathas ambaye alicheza mechi yake ya kwanza tangu alipojiunga na klabu hiyo. Siku ya Jumamosi, Robert Lewandowski aliwapa mabingwa watetezi Bayern Munich ushindi wa 2-0 dhidi ya Werder Bremen.

1. FC Rielasingen-Arlen v Borussia Dortmund - DFB Cup
Dortmund waliendelea na maisha bila ya DembelePicha: Getty Images/A.Pretty

Borussia Dortmund wanashikilia usukani wa Bundesliga, kwa tofauti ya mabao, baada ya ushindi wa 2-0 nyumbani dhidi ya Hertha Berlin. Mabao yalifungwa na Pierre-Emerick Aubameyang na Nuri Sahin. "huu ni wakati mzuri sana. Tun ataka kushinda mechi zetu, tunataka kulifurahia kandanda letu, tunataka kutawala mchezo ugenini na nyumbani. Na naamini tumefanikiwa vizuri sana katika mechi mbili za kwanza"

Aubameyang na Lewandowski wana mabao sita kila mmoja baada ya kucheza mechi nne katika mashindano yote, lakini Lewandowski anaongoza katika Bundesliga akiwa na matatu dhidi ya mawili ya Auba. Kama tu Dortmund na Bayern, Hamburg pia walishinda mechi zao mbili za ufunguzi baada ya kuwabwaga Cologne kwa mabao matatu kwa moja.

Kwingineko, Wolfsburg walipata ushindi wa moja bila dhidi ya Eintracht Frankfurt bao lililotiwa kimyani na Daniel Didavi. Andries Jonker ni kocha wa Wolfsburg "bila shaka kama mechi ya kwanza ya ufunguzi nyumbani inakamilika kwa kichapo na hali ya kukata tamaa, basi ukishinda inayofuata inakuwa raha. Hakuna michuano rahisi ya ugenini katika Bundesliga na hasa hapa Frankfurt

Hoffenheim walipambana na kutoka sare ya 2-2 na Bayer Leverkusen. Borussia Moenchengladbach walitoka sare ya 2-2 na Augsburg.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Abdulrahman