1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano bado yanaedelea Sudan Kusini

Mjahida24 Agosti 2016

Sudan inasema kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar, yupo mjini Khartoum kwa ajili matibabu baada ya kukimbia nchini mwake akivitoroka vikosi vya serikali ya Rais Salva Kiir.

https://p.dw.com/p/1Jo9c
Kiongozi wa upinzani Sudan Kusini Riek Machar
Kiongozi wa upinzani Sudan Kusini Riek MacharPicha: picture-alliance/dpa/Stringer

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Sudan, SUNA, Riek Machar ataendelea kubakia nchini Sudan kadiri matibabu yake yatakavyohitaji.

"Sudan imempokea Riek Machar kwa sababu za kiutu hasa kwa sababu ya mahitaji yake ya matibabu. Hali yake kwa sasa ni imara na atabakia nchini humu kwa matibabu hadi wakati atakapotaka kuondoka kuelekea kule anakokutaka kukamilisha matibabu yake" alisema Waziri Osman.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir alimfuta kazi Riek Machar katika nafasi yake ya makamu wa rais baada ya mapigano mjini Juba kuzuka upya mwezi uliyopita kati ya vikosi vitiifu kwa mahasimu hao wawili wa muda mrefu. Mapigano yanayoendelea Sudan Kusini yamewalazimu maelfu ya watu kuikimbia nchi hiyo.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa upinzani Riek Machar
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa upinzani Riek MacharPicha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Machar alikuwa amekimbilia msituni baada ya mapigano mapya kutokea mjini Juba na baadaye mwezi huu, akapata msaada kutoka kwa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO, akiwa na jeraha mguuni. Baadaye msemaji wake alisema Machar ameondoka Sudan Kusini kuvikimbia vikosi vya Kiir na kwamba jeraha lake halikuwa baya sana.

Hata hivyo msemaji huyo aliyeko mjini Nairobi, James Gatdet Dak, hakuweza kupatikana kuthibitisha uwepo wa Machar mjini Khartoum. Awali James Dak alisema mpango wa Machar ulikuwa ni kwenda mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambako kumekuwa kukiandaliwa mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini.

Waziri John Kerry ahimiza pande hasimu zitekeleze mpango wa amani

Machar na Kiir wamekuwa mahasimu wa muda mrefu hata kabla ya taifa hilo changa duniani kujipatia uhuru wake mwaka wa 2011 ambapo wote walikuwa makamanda katika jeshi la SPLA lililoiyondoa serikali ya Sudan. Lakini ilipofika Desemba mwaka 2013 mzozo wa kisiasa kati ya kabila la Kiir la Dinka na Machar la Nuer ukawaka moto na kusababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalio ndani ya misingi ya kikabila.

Baadaye wawili hao walitia saini mkataba wa amani mwaka wa 2015 uliyopelekea Machar kurejea mjini Juba mwezi Aprili kuchukua tena nafasi yake kama Makamu wa rais, lakini mapigano yakazuka tena mwezi uliyopita na kufutwa katika cheo hicho.

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters/J. Roberts

Kwa upande mwengine wakati wa ziara yake nchini Kenya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amezihimiza pande hizo mbili hasimu zitekeleze mpango wa amani au wakabiliwe na vikwazo kutoka Umoja wa Mataifa.

Huku hayo yakiarifiwa watu 275 wameripotiwa kuuwawa katika mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi Sudan Kusini hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa pande zote mbili hasimu. Gavana wa Jonglei Phillip Aguer amesema waasi wameishambulia kambi yakijeshi Kaskazini Mashariki mwa mji wa Pajut mnamo Agosti 19 na kusababisha mauaji ya watu 242 kutoka upinzani, wanajeshi 23 wa serikali na raia 10.

Lakini kwa upande wake msemaji wa waasi, James Gatdet, amesema jeshi lilianzisha mashambulizi na kwamba zaidi ya wanajeshi 300 waliuwawa pamoja na waasi takriban 30.

Mwandishi: Amina AbubakarAP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef