1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti: Mashambulizi ya Taliban yanaongezeka

1 Februari 2021

Ripoti mpya iliyotolewa nchini Marekani inasema mashambulizi ya kundi la Taliban kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, yanaongezeka huku mauaji ya kupangwa yanawalenga watu maalum.

https://p.dw.com/p/3of6C
 Afghanistan Journalist Autobombe Anschlag Taliban
Picha: Abdul Khaliq/AP/dpa/picture alliance

Ripoti hiyo ya shirika liitwalo SIGAR linalofuatilia mabilioni ya dola yanayotumiwa na Marekani katika juhudi za kuijenga upya Afghanistan imesema mashambulizi yaliyotekelezwa na kundi la Taliban kwa mwaka 2020 yamepindukia idadi ya mwaka 2019 na mji mkuu Kabul ndiyo umekuwa kitovu cha hujuma za wanamgambo hao.

Ikinukuu takwimu zilizokusanywa na vikosi vya jeshi la Marekani nchini Afghanistan, ripoti ya SIGAR imeainisha jinsi wanamgambo wa Taliban walivyozidisha mashambulizi yao mjini Kabul hasa katika robo ya mwisho ya mwaka uliopita.

Wanamgambo wa Taliban walitekeleza mfululizo wa mashambulizi nchini Afghanistan Disemba iliyopita ikiwemo katika jimbo la kaskazini la Baghlan na la kusini la Uruzgan ambayo ndani ya siku mbili pekee yaliwauwa wanajeshi 19 wa jeshi la taifa hilo.

Ndani ya mwezi huo huo, mjini Kabul, bomu la kutegwa barabarani liliripua gari na kujeruhi watu wawili huku katika kisa kingine mwanasheria mmoja aliuwawa kwenye shambulizi la kulengwa.

Orodha ya vifo na majeruhi inatisha 

Afghanistan Unabhängigkeitstag 18.8.2019
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Maqbool

Takwimu zilizorikodiwa na ujumbe wa msaada wa Jumuiya ya kujihami NATO nchini Afghanistan zinaonesha kuwa watu 810 walikufa na wengine zaidi ya 1,776 walijeruhiwa nchini Afghanistan kati ya Oktoba mosi hadi Disemba 31 mwaka jana. Tarakimu hizo zimeorodheshwa pia kwenye ripoti ya SIGAR.

Kwa jumla takwimu zilizokusanywa zinaonesha kwamba madhara yaliyosababishwa na mabomu yanayotegwa na kundi la Talibanyameongezeka kwa asilimia 17 baina ya mwezi Oktoba na Disemba mwaka jana.

Hata hivyo licha ya kiwango cha mashambulizi kuongezeka, idadi ya waliokufa au kujeruhiwa imepungua kwa asilimia 14 ikilinganishwa na robo ya tatu ya mwaka 2020 yaani kati ya mwezi Julai hadi Septemba.

Marekani kudurusu upya mkataba wake na Taliban 

Ripoti ya SIGAR imetolewa katika wakati utawala mpya mjini Washington chini ya rais Joe Biden unalenga kutizama upya mkataba yaliyofikiwa kati ya Marekani na kundi la Taliban na kutiwa saini Februari iliyopita na serikali ya Donald Trump.

DW Special 20 Jahre Bundeswehreinsatz in Afghanistan
Picha: picture-.alliance/dpa/M. Gambarini

Marekani imekuwa muungaji mkono mkubwa wa serikali ya Afghanistan tangu ilipoivamia nchi hiyo muda mfupi baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 na kuungusha utawala wa kundi la Taliban waliokuwa wakiongoza taifa hilo na kutuhumiwa kutoa hifadhi kwa kiongozi wa Al-Qaeda Osama bin Laden.

Licha ya juhudi za miaka ya karibuni ya kuimarisha nguvu ya serikali mjini Kabul, bado imekuwa vigumu kuijenga upya Afghanistan ambayo imeharibiwa kwa vita na mifumo mingi ya utawala imeparaganyika.

Hivi sasa mazungumzo yanayosuasua kati ya kundi la Taliban na serikali ya Afghanistanyanaendelea nchini Qatar na yanabeba matumaini ya kufikiwa makubaliano yatakayomaliza mapigano na kuijenga upya Afganistan.