Ripoti ya ILO yaonya kuhusu hali mbaya ya maisha katika mamlaka ya Palestina.
29 Mei 2007Sehemu ya jamii inayoishi chini ya kiwango cha umasikini imeongezeka kwa asilimia 26 kati ya March 2006 na March 2007, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Jumatatu, ambayo iko chini ya msingi wa uchunguzi wa ujumbe wa ngazi ya juu uliotumwa na shirika la kazi la kimataifa ILO mwezi Aprili nchini Israel na maeneo yaliyovamiwa ya Waarabu.
Pato la jumla la taifa la kila mwaka GDP, limepungua kwa asilimia 40 katika maeneo hayo kati ya 1999 na 2006.
Saba kati ya kaya 10 , ambazo zina kiasi cha watu milioni 2.4 , zinaishi katika umasikini katika maeneo yanayokaliwa kimabavu na Israel, inasema ripoti hiyo, ambayo itadurusiwa tena katika kikao cha May 30 hadi Juni 15 cha shirika hilo la kimataifa, kinachofanyika kila mwaka mjini Geneva.
Ni mmoja tu kati ya watu watatu katika maeneo hayo anafanyakazi, wakati wawili kati ya watu watatu hawana ajira, ama kutokana na kwamba hawakuajiriwa ama kwasababu wako nje ya kundi linalofanyakazi, inasema sehemu moja ya ripoti hiyo.
Kiasi cha watu 206,000 hawana ajira, ikiwa ni sawa na asilimia 24 ya kundi lote la watu wanaoweza kufanyakazi.
Mkurugenzi wa shirika la ILO Juan Somavia amesema kuwa hali katika maeneo yanayokaliwa na Israel ni mbaya. Ghasia hazijasita, na zinaendelea kuwaathiri Wapalestina na Waisreal, licha ya kuwa ni katika viwango tofauti, amesema.
Miaka 40 ya Israel kukalia maeneo ya Ukingo wa magharibi, ukanda wa Gaza na milima ya Golan sio sababu ya pekee ya kuporomoka kwa hali hiyo hivi sasa katika eneo hilo, inasema ripoti hiyo, ambayo pia inadokeza kuhusu hatua mbali mbali zilizochukuliwa baada ya uchaguzi na kusababisha kubadilika kwa uongozi wa serikali katika mamlaka ya Palestina March 2006.
Uchaguzi wa januari 2006 ulileta ushindi kwa chama cha Hamas , ambacho kinamsimamo mkali zaidi katika upinzani wake dhidi ya Israel na mataifa ya magharibi ambayo yanaisaidia. Chama chenye msimamo wa kati cha Fatah kilikuwa na udhibiti wa serikali ya mamlaka ya Palestina tangu mwaka 1994.
Mgomo dhidi ya kuipatia serikali ya Palestina inayoongozwa na chama cha Hamas msaada wa kifedha wa mataifa ya magharibi, umesababisha athari kubwa kwa Wapalestina na uchumi wa mamlaka hiyo, inasema ILO.
Athari hizo ziliongezeka kutokana na uzuiaji wa Israel wa fedha za kodi katika mamlaka hiyo, hali ambayo imesababisha kupungua kwa pato la wastani la kila mwezi la dola milioni 60.
Kiongozi wa ILO amesema kuwa sababu kuu ya matatizo ya kijamii na kiuchumi inaletwa na utaratibu wa kufungwa maeneo hayo pamoja na uthibiti, ikiwa ni pamoja na ukuta unaojengwa na Israel unaotenganisha.
ILO inaonya kuwa mfumo wa kijamii katika maeneo yanayokaliwa kimabavu na Israel uko katika mbinyo wa hali ya juu kutokana na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira, hususan miongoni mwa vijana , pamoja na kiwango cha juu cha umasikini na ghasia, ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa utawala wa sheria.