RIPOTI YA SHIRIKA LA BIASHARA DUNIANI (WTO)
18 Januari 2005SHIRIKA LA BIASHARA DUNIANI (WTO)
Ukaguzi uliopenedekezwa kufanywa na Shirika la Biashara Duniani –World Trade Organisation (WTO) miaka 10 tangu kuasisiwa kwake,umependelea mno kupanua biashara dunianii na umezitaka serikali kuchangia kwa nguvu kukuza biashara kati ya nchi mbali mbali au pande mbali mbali kuliko zile kati ya nchi mbili au za kimkoa.
Wakati huo huo wakosoaji wa mfumo sasa wa biashara wanadai kwamba Shirika la WTO lenye makao yake mjini Geneva,Uswisi,kimsingi, limedhofisha vita vya kupambana na umasikini duniani.Wanaamini kwamba, mfumo wa biashara wa shirika la WTO kimsingi, umeyanufaisha makampuni makubwa ya nchi za kiviwanda na matajiri wachache sehemu mbali mbali duniani bali si masikini.
Ripoti ya jumatatu ya wiki hii,iliotungwa na kikundi cha wataalamu wa kiuchumi chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa zamani wa Shirika hili la WTO Peter Sutherland, inasema kufunguliwa milango ya masoko na kuondoshwa vikwazo vya kibiashara kungali kukitoa kwa ulimwengu matumaini bora kabisa ya kukuza uc humi tena tangu kwa nchi zilizoendelea na hata kwa nchi changa.
Ripoti hii ya kurasa 90 inayataka mataifa kuafikiana juu ya muda maalumu wa kuchukua hatua ya pamoja ya kuondoa ushuru wa forodha na vikwazo vya biashara.
Bw.Sutherland ambae ni Kamishna wa zamani wa biashara wa Umoja wa Ulaya,aanapendekeza katika ripoti yake kuwa WTO iitishe mkutano maalumu wa kilele kila baada ya miaka 5 ili kulitilia nguvu Shirika la WTO ambalo limekuwa likikosolewa sana na nchi changa na baadhi ya wanauchumi.
Ripoti hii halkadhalika inasisitiza mno juu ya miradi mikubwa ya biashara na kiuchumi inayojumuisha mataifa mbali mbali kwa pamoja pamoja na kutekelezwa kwa ile ilioitwa AGENDA YA DOHA ya mwaka 2001.
Ripoti hii iliopendekezwa itungwe na mkurugenzi wa sasa wa Shirika hili la Biashara (WTO) Supachai Panitchpakdi,inaitisha pia kuwapo hali ya uwazi zaidi na hasa upande wa mapendekezo yake ya kuufikia umma hadharani na kwa Jumuiya za kiraia.Inaitisha mikutano wazi ifanyike kutatua migogoro na kuwapa wajumbe na raia fahamu bora ya mfumo wa biashara duniani.
Makisio haya katika ripoti hii yamekuja huku Shirika la Biashara Duniani (WTO) likiadhimisha mwaka wa 10 tangu kuasisiwa na siku tu kabla ya kufanyika kwa mkutano usio rasmi wa mawaziri wa biashara huko Davos, Uwsisi ili kuyatilia nguvu yale mazungumzo yaliozorota ya Doha,Gatar.
WTO –shirika lililoundwa Januari mosi,1995 linachangia mno katika kurekebisha na kuongoza mahusiano ya kibiashara duniani. Lina jumla ya wanachama 148 na linaegemea msingi wa mapatano ya biashara huru na raslimali ambayo yamewapa watiaji raslimali ulimwenguni dhamana zenye lengo la kuhimiza raslimali kutoka nje na nyendo za viwanda mbali mbalo kote duniani na hasa kutoka Marekani na Ulaya katika nchi ambazo ujira uko chini mfano wa China na Mexico.
Kwa jumla, Marekani imeikaribisha ripoti hii na inadai imethibitisha msimamo wake kuwa biashara chini ya mfumo unaojumuisha nchi nyingi au pande mbali mbali,ndio njia bora za kukuza uchumi ulimwenguni.
Shirika la biashara la dunia limekumbwa hata hivyo na matatizo kadhaa wa kadha:Mvutano uliibuka kati kati ya Agenda yaDoha ya maendeleo huko cancun,Mexico 2003.Nchi nyingi zinazoinukia ,wanauchumi na vikundi huru vinavyohimiza maendeleo zimezusha maswali makali juu ya mustakbala wa Shirika hili la WTO zikidai upinzani unaoongezeka kupinga Agenda yake kunaonesha ufa mkubwa uliopo katika mfumo wake.
Biashara duniani inayotia maanani kuwa idadi kubwa ya wanadamu katika nchi zisizoendelea wanaishi katika hali mbaya ya ufukara kama ilivyochambuliwa na Banki Kuu ya Dunia -–aani wakaazi wake wakivuna si zaidi ya dala 1 kwa siku, wamezidi kuongezeka kila kukicha tangu kuasisiwa kwa Shirika hili-kwa muujibu wa tarakimu za banki Kuu ya Dunia.
Mafanikio makubwa yalioonekana katika kupiga vita ufukara katika nchi changa yamedhihrika katika nchi kama China na India-nchi mbili zinazochukua njia tofauti kabisa na mapendekezo ya Shirika hili la WTO katika sera zao.