Ripoti ya shirika la Umoja wa mataifa la UNDP yachapishwa mjini New York
5 Novemba 2010Ripoti ya shirika la Maendeleo la Umoja wa mataifa UNDP iliyochapishwa jana,inazungumzia maendeleo jumla ingawa inahofia mabadiliko ya hali ya hewa yasije yakachafuwa matarajio ya siku za mbele.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ya shirika la maendeleo la Umoja wa mataifa UNDP,hali ya elimu,afya na pato imeimarika katika nchi nyingi za dunia huku Oman na jamhuri ya Umma wa China zikifanya vizuri zaidi.
Hata hivyo Norway inaendelea kushikilia usukani katika ripoti ya mwaka ya maendeleo ya shirika hilo, huku Zimbabwe ikiburura mkia na kurithi nafasi iliyokuwa ikishikiliwa hapo awali na Niger.
Nchi 169 tuu kati ya 192 wanachama wa umoja wa mataifa, ndizo zilizoorodheshwa katika ripoti hiyo. Nchi zilizosalia,ikiwa ni pamoja na Korea ya kaskazini, wachunguzi wa shirika la UNDP hawakupatiwa maelezo yoyote waliyokuwa wakiyataka.
Ujerumani inakamata nafasi ya kumi huku Marekani ikipanda kutoka nafasi ya 13 mwaka jana na kushikilia nafasi ya nne mwaka huu.
Faharasa ya maendeleo iliyowekwa na shirika la maendeleo la Umoja wa mataifa na ambayo inatilia maanani pato,afya na elimu inaonyesha maendeleo makubwa yaliyopatikana kuwanzia kiwango cha sifuri nukta 57 mwaka 1990 na kufikia sifuri nukta 68 mnamo mwaka huu wa 2010.
Nchi tatu tuu,Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,Zambia na Zimbabwe hazikupiga hatua mbele katika sekta hizo,ikilinganishwa na mwaka 1970.
Ama kwa upande wa Tanzania na kwa mujibu wa mtaalam wa kiuchumi wa shirika la UNDP mjini Daresalam, Amara Kuun Bandara,hali imeboreka nchini humo ikilinganishwa na mwaka jana.Itafaa kusema hapa kwamba Tanzania imeorodheshwa nafasi ya 148 kati ya 169 ikitanguliwa na Uganda, nafasi ya 143, visiwa vya Comoro nafasi ya 140 na Kenya nafasi ya 128.
Ni katika eneo la Asia na Pacific ambako maendeleo yalikuwa ya kasi na kufuatiwa na Asia ya kusini na mataifa ya kiarabu.
Mwandishi: Hamidou/Reuters,Afp
Mpitiaji: Josephat Charo