Ripoti ya SIPRI yabainisha ongezeko la uuzaji silaha duniani
11 Desemba 2017Ripoti hiyo ya SIPRI imebainisha kuwa huku walionufaika pakubwa ni kampuni za silaha za Marekani na Ulaya Magharibi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyozinduliwa leo, biashara ya silaha duiani na huduma za kijeshi, vimeongezeka tena kwa mwaka 2016 ikiwa ni mara ya kwaza katika kipindi cha miaka mitano. Biashara ya silaha imeongezeka kwa asilimia 1.9 ukilinganisha na mwaka jana na kwa asilimia 38 ukilinganisha na 2002.
Takwimu
Takwimu hizo mpya zinasema kuwa kwa mwaka 2016 mashirika makubwa 100 ya utengenezaji wa silaha yaliuza silaha na mifumo ya kisilaha ya takribani dola 374.8 bilioni. Kampuni za kutengeneza na kuuza silaha zipo hasa hasa Marekani. Kadhalika ripoti hiyo imesema uuzwaji wa silaha katika kampuni za Marekani, ulipanda kutoka asilimia 4 kwa mwaka 2016 ikiwa ni sawa na jumla ya dola za Kimarekani bilioni 217. Lakini sababu sio kuwepo wa majeshi ya Marekani katika nchi nyingine. Inaelezwa kuwa takwimu hizo ziliongezeka kutokana na manunuzi ya mifumo mikubwa ya silaha yaliyofanywa na nchi nyingine.
Kampuni kubwa ya utengenezaji wa silaha duniani, LOCKHEED MARTIN; ilipata faida kubwa kwa kuziuzia nchi kama Uingereza, Italia na Norway silaha ya mpya ya F-35. Hata hivyo wateja wake wakubwa ni jeshi la Marekani, Air Force. Kampuni hiyo ya Lockheed Martin, ni miongoni mwa kampuni 100 zilizofanyiwa utafiti na wataalamu wa SIPRI. Kwa mara nyingine tena, ripori inaonyesha kwa uhalisia kuwa silaha nyingi zinatengenezwa katika kampuni za Marekani. Kampuni za Marekani zinauza asilimia 57.9 ya silaha zote zinazouzwa duniani.
Ulaya Magharibi, inashika nafasi ya pili katika orodha hiyo kwa kuuza silaha, ikifuatiwa na Urusi, inayouza silaha kwa asilimia 7.1 duniani kote.
Migogoro inatajwa kuchochea uuzwaji wa silaha
Wakati huo kampuni za Ufaransa na Italia, zinauza silaha kwa kiasi kidogo. Licha ya Uingereza kutaka kujitoa katika Umoja wa Ulaya, lakini biashara ya silaha nchini humo imeongezeka na Ujerumani pia.Kwa mfano, kampuni ya kijerumani ya kutengeneza vifaru vya kijeshi ya Krauss-Maffei, na Rheinmetall, inayotengeneza magari ya kivita, ilipata faida kutokana na wingi wa mahitaji kutoka Ulaya, Mashariki ya kati na Kusini-Mashariki mwa Asia.
"Hata hivyo ni vigumu kuonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya ununuzi mkubwa wa silaha na vita vinavyoendelea. Lakini hata hivyo kuna uhusiano. Kuna mahitaji makubwa ya silaha za aina fulani, makombora, magari ya ardhini, kwa mfano," Aude Fleurant, Mkurugenzi katika taasisi ya SIPRI amesema.
Hata hivyo Korea ya Kusini, inajitengenezea silaha zake yenyewe . Mwaka 2016 kampuni ya Korea Kusini, iliripotiwa kuongeza mauzo ya silaha kwa asilimia 20.6.Watengenezaji wa silaha Korea Kusini, ambao wanauza kwa ajili ya wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, wanazalisha faida kwa njia hiyo tu.
Nchi nyingine zinazotajwa kuwa watengenezaji wakubwa wa silaha ni China. Hata hivyo, ripoti hiyo haina takwimu zozote za nchi hiyo. Lakini Fleurant anaamini kuwa China ni miongoni mwa nchi 20 zenye kampuni kubwa za silaha. Ripoti hiyo mpya ya SIPRI inatoa taarifa ya nani anauza au kununua silaha nyingi zaidi lakini pia, inaonyesha ni kwa namna gani dunia kwa ujumla wake, iko salama kwa sasa.
Mwandishi: Florence Majani/dw
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman