1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robo ya watoto duniani wanaishi katikati ya vita

10 Julai 2018

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto, UNICEF, imesema robo ya idadi ya watoto duniani, ambao ni sawa na karibu watoto milioni 535 wanaishi kwenye mataifa yaliyoathiriwa na mizozo na majanga.

https://p.dw.com/p/3183A
Syrien Krieg - Kind in Rakka
Picha: picture-alliance/AP Photo/Jonathan Hyams, Save the Children

UNICEF limeangazia watoto wanaoishi kwenye mataifa yanayokabiliwa na mizozo ambayo ni pamoja na Yemen, Mali na Sudan Kusini. 

Mkuu wa shirika hilo la UNICEF, Henrietta Fore ameliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwenye kikao kilichojadili masuala ya watoto katika maeneo yanayokabiliwa na vita kwamba takriban mtoto mmoja kati ya wanne hujikuta katikati ya hali hiyo.

Aliwaangazia watoto na vijana wadogo ambao maisha yao yameharibiwa na mizozo, katika baadhi ya mataifa yenye vita kama Yemen, Mali na Sudan Kusini. Aliangazia pia vijana wadogo wanaopewa mafunzo ya kijeshi, waliouawa kwa mabomu ya kufukiwa ardhini ama hata walioshambuliwa wakiwa shuleni na kupoteza matumani si tu ya mustakabali wao wa kimaisha bali pia wa mataifa yao. 

Sweden, ambayo ni mwenyekiti wa mwezi wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, imeandaa kikao hicho cha wazi chenye maudhui "kuwalinda watoto leo, zuia machafuko kesho" na kuunga mkono azimio lililopitishwa kwa kauli moja na wanachama wake 15 ili kuimarisha hatua za Umoja wa Mataifa za kuhakikisha watoto wanalindwa.

Schweden Stockholm Stefan Lofven
Waziri mkuu wa Sweden Stefan Lofven asema watoto takriban milioni 350 wameathirika na vita na mizozo.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Simander

Waziri mkuu wa Sweden Stefan Lofven aliyeongoza kikao hicho, alisema hakuchukuliwi hatua za kutosha katika kuwalinda watoto. Alisema na kusisitiza kwamba watoto milioni 350 wameathirika kwenye maeneo yenye mizozo hii leo. 

Lofven amesema azimio hilo pia kwa mara ya kwanza linasisitiza kuhusu mahitaji na mazingira hatarishi kwa watoto wa kike na wa kiume ambayo yanatofautiana. Aidha, amesisitiza kuhusu upatikanaji wa elimu kwa watoto hao, pamoja na huduma za afya ya mwili na akili.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataiofa kuhusu watoto waliopo kwenye maeneo ya vita na mizozo, Virginia Gamba kwa upande wake ameelezea kushtushwa na idadi ya visa vya ukiukwaji wa haki za watoto kwa mwaka 2007, vilivyofikia 21,000, vilivyoripotiwa hivi karibuni na Umoja wa mataifa, ambavyo vimeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2016.

Amesema idadi hiyo ni ya kutisha, na kuzungumzia umuhimu wa kuungana pamoja kuchukua hatua za kubadilisha wimbi hilo la kihistoria, hususan kwa kuangazia namna ya kuzuia na kuwaunganisha na jamii ili kuvunja mzunguko wa ukatili dhidi ya watoto.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley ameliambia baraza hilo kwamba zaidi ya asilimia 60 ya watu katika maeneo yanayokabiliwa na mizozo wako chini ya miaka 25.

Amesititiza umuhimu wa elimu kama njia ya kuponyesha majeraha yaliyosababishwa na mizozo, lakini akionya kwamba watoto wanaokua bila ya kuwa na elimu wala ujuzi, watakuwa walengwa muhimu watakaopewa mafunzo ya kijeshi na makundi ya itikadi kali na yaliyojihami kwa silaha.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE.

Mhariri:Yusuf Saumu