1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Waasi wa RSF kufungua njia salama katika mji wa al-Fashir

18 Mei 2024

Kikosi cha wanajeshi waasi cha RSF nchini Sudan kimetangaza nia yake ya kufungua eneo litakalotumika kama njia salama nje ya mji wa bandari wa al-Fashir huko Kaskazini mwa Darfur.

https://p.dw.com/p/4g1nu
Sudan | RSF
Picha: Mohamed Babiker/Photoshot/picture alliance

Kikosi hicho cha RSF, kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Daglo kinapambana na jeshi la serikali linalomuunga mkono kiongozi wa kijeshi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Soma Pia:UN yaonya uwezekano wa janga la kibinadamu al Fashir  

RSF imethibitisha katika chapisho lake kwenye mtandao wa X kwamba vikosi vyake viko tayari kuwasaidia raia kwa kufungua njia salama ili waweze kuondoka kwa hiari yao na kwenda kwenye maeneo mengine watakayochagua na wanajeshi hao wa RSF wameahidi kuwapa ulinzi raia.

Sudan | Mohamed Hamdan Daglo
Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, kiongozi wa RSF, kikosi kilichoasi nchini SudanPicha: Ashraf Shazly/AFP

Mji wa al-Fashir, ulio Kaskazini mwa jimbo la Darfur ni eneo ambalo wakati mmoja lilikuwa ni kitovu muhimu cha misaada ya kibinadamu kwa watu wengi waliokusanyika huko lakini kwa sasa umekuwa katika vita vikali ambapo waasi wa RSF wamekuwa wakitaka kuudhibiti.

Wanajeshi hao wa RSF wametoa wito kwa wakaazi wa al-Fashir kuepuka maeneo yenye mizozo na maeneo ambayo yanaweza kulengwa na vikosi vya anga na pia wamewataka wakaazi wa eneo hilo kuwa macho ili wasiingizwe kwenye vita.

Umoja wa Mataifa I Volker Türk
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa mataifa Volker TurkPicha: Martal Trezzini/dpa/picture alliance

Soma Pia:Zaidi ya watu milioni 7 kukabiliwa na njaa Sudan Kusini  

Siku ya Alhamisi Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa mataifa Volker Turk alisema tayari ameshafanya majadiliano na makamanda wa pande zote mbili zinazohasimiana nchini Sudan na pia alieleza wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuibuka kwa janga la kibinadamu iwapo mji wa al Fashir utashambuliwa.

Msemaji wa Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani, amearifu kuwa Turk amesema mapigano katika eneo hilo yatazidisha mzozo kwa jamii na kusababisha matokeo mabaya kwa raia.

Mzozo wa Sudan

Sudan imekuwa katika mzozo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kati ya jeshi la serikali linaloongozwa na kiongozi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan na kikosi cha waasi cha RSF kinachoongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.

Soma  Pia:Marekani yaonya uwezekano wa mauaji ya kimbari Sudan  

Kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa, mzozo huo umesababisha vifo vya takriban watu 15,000 katika mji wa El-Geneina ambao ni mji mkuu wa jimbo la magharibi la Darfur.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF)mnamo siku ya Jumatano lilisema hospitali yake huko Darfur Kaskazini ilipokea miili ya watu zaidi ya 450 waliouawa katika mapigano hayo ya tangu Mei 10, lakini shirika hilo limesema kuwa idadi halisi ya watu waliouawa huenda ikawa kubwa zaidi.

Darfur Sudan Kina mama na watoto
Mama na mwanawe juu ya Punda wanaoishi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk katika mji wa al- FashirPicha: ASHRAF SHAZLY/AFP

Maelfu ya watu wameuawa na wengine mamilioni wameyakimbia makazi yao tangu vita vilipoanza mwezi Aprili mwaka 2023.

Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa ulionya kuwa ulikuwa na asilimia 12 pekee ya dola bilioni 2.7 ilizotafuta kwa ajili ya Sudan, nchi iliyoathiriwa vibaya na vita huku janga la njaa nalo likizidi kujongea.

Chanzo:AFP