1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rupiah Banda aapishwa rasmi kuwa Rais wa Zambia.

Nyanza, Halima2 Novemba 2008

Kaimu Rais wa Zambia, Rupiah Banda ameapiashwa rasmi leo, kuwa Rais wa Zambia baada ya kutangwazwa rasmi kuwa mshinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika Alhamisi nchini humo.

https://p.dw.com/p/Fm9c
Aliyekuwa Rais wa Zambia, marehemu Levy Mwanawasa, kifo chake kimesababisha kuchaguliwa kwa Rais mpya wa nchi hiyo Rupiah Banda.Picha: AP

Bwana Banda ameshinda nafasi hiyo, baada ya kupata asilimia 40.1 dhidi ya mpinzani wake Michael Sata aliyepata asilimia 38.1 ya kura milioni 1.79 zilizopigwa katika uchaguzi uliofanyika siku ya Alhamis.

Hata hivyo, upinzani nchini humo umekataa kuyatambua matokeo hayo, yalioonesha kwamba Bwana Banda ameshinda uchaguzi.

Msemaji wa Chama kikuu cha upinzani nchini Zambia, cha The Patriotic Front, Given Lubinda amesema kesho wataiomba mahakama itoe idhini ya kufanyika kwa uchunguzi pamoja na kurudia kuhesabu upya kura hizo zilizopigwa.

Chama hicho cha upinzani kinadai kuwa uchaguzi wa Alhamis wiki hii, ulikuwa na undanganyifu na kimewataka maafisa wa uchaguzi kusitisha kutangaza matokeo zaidi ya uchaguzi.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Zambia limewekwa katika hali ya tahadhari ili kudhibiti ghasia zozote zinazoweza kutokea, kufuatia ghasia zinazodaiwa kufanywa na wafuasi wa upinzani kupinga ushindi wa Bwana Banda.

Uchaguzi wa Rais nchini Zambia umefanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Levy Mwanawasa, kufariki dunia Agosti mwaka huu, kutokana na ugonjwa wa kiharusi.