1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto aitaka tume ya IEBC kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru

Wakio Mbogho11 Februari 2022

Naibu Rais wa Kenya Wiliam Ruto ameitaka tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kuuhakikishia umma kwamba uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu utakuwa huru na wa haki.

https://p.dw.com/p/46tBY
Kenia Präsident William Ruto
Picha: picture-alliance/Photoshot/P. Siwei

Wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanzakwa mara nyingine tena wanapiga kampeini katika kaunti ya Nakuru wakiongozwa na naibu Rais Wiliam Ruto. Ruto amewakosoa wenzake kwa kueneza propaganda kuhusu wizi wa kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Wakati huo huo, mahakama ya juu jijini Nakuru imemuachia huru mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka ya matamshi ya chuki dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mama yake ambaye ni mke wa Rais wa kwanza wa Kenya Mama Ngina Kenyatta. Septemba mwaka 2020, mbunge huyu alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka matano yakiwemo matamshi ya chuki, kumshambulia afisa wa polisi na kumiliki silaha haramu.

Wahlen in Kenia 2017 - Kampagne von Uhuru Kenyatta
Uchaguzi uliopita, Ruto alikuwa mrengo mmoja na rais Uhuru KenyattaPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Sudi ambaye ni mfuasi sugu wa naibu Rais Ruto ameupongeza uamuzi huu wa mahakama kama uthibitisho wa uhuru unaohitajika, hasa wakati huu taifa linaposhuhudia joto la kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu.

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i ni kati ya viongozi wa kitaifa wanaomkosoa Naibu Rais  Ruto na wandani wake, kwa kile wanachokiita kueneza uongo kuhusu utendaji kazi wa serikali ya Jubilee, serikali ambayo imewapa mamlaka walio nayo.

Kadhalika, kundi la wanawake wa chama cha ODM wanaomuunga mkono kinara wa chama hicho Raial Odinga, hii leo wametangaza msururu wa mipangilio walio weka ya kumpigia debe kiongozi huyo.

Haya yanajiri siku moja baada ya vuguvugu la azimio la wanawake kuzinduliwa. Waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa na viongozi wa magharibi mwa Kenya wanaomuunga mkono Raila Odinga wanaendeleza kampeini za muungano wa Azimio la umoja mjini Kakamega na vitongoji vyake.