Rwanda yaadhimisha miaka 30 ya mauaji ya kimbari
8 Aprili 2024Miaka 30 baada ya mauaji hayo ya kimbari nchini Rwanda, raia nchini humo Jumapili walikusanyika katika mji mkuu Kigali huku wakibeba mishumaa kuwakumbuka waliouawa.
Kwa kuzingatia tamaduni, Rais Kagame aliweka mashada ya maua kwenye makaburi ya wahanga hao na kuwasha mwenge wa ukumbusho katika eneo la makumbusho ya mauaji hayo ambapo zaidi ya waathiriwa 250,000 wanaaminika kuzikwa.
Kagame asema Rwanda haitosahau mauaji ya kimbari
Akihutubia umati uliohudhuria hafla hiyo uliowajumuisha wakuu wa nchi za Afrika na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, Rais Kagame alisema kuwa Rwanda ilifedheheshwa sana na ukubwa wa hasara iliyopata na kwamba mafunzo waliyopata yatakumbukwa daima.
Soma pia:Wiki ya kumbukumbu ya mauwaji ya kimbari nchini Rwanda
Rais Kagame aliongeza kuwa ni jamii ya Kimataifa iliyoshindwa kuisaidia nchi hiyo aidha kutokana na dharau ama uoga.
Rais Macron asisitiza kuhusu jukumu la Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda
Katika ujumbe aliotoa kupitia njia ya vidio, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisisitiza kuhusu maoni aliyotoa mnamo Mei 2021 wakati alipokiri kuhusu jukumu la Ufaransa katika mauaji hayo ya halaiki na kushindwa kuzingatia maonyo ya hatari ya mauaji hayo ya kimbari lakini hakuomba msamaha rasmi.
Macro ameongeza kwamba anamshukuru Rais Kagame kwa kuyapokea vizuri maneno yake na kwamba hatua hiyo inafungua ukurasa mpya katika mahusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais wa Halmashauri Kuu ya AU asema hakuna anayeweza kujitetea kwa kutowajibika wakati wa mauaji ya Rwanda
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema kuwa kushindwa kwa Jumuiya ya kimataifa kuingilia kati, kumekuwa sababu ya aibu inayoendelea na kuongeza kwamba hakuna mtu hata Umoja huo wa Afrika unaoweza kujieteta kwa kutochukuwa hatua.
Soma pia: Ufaransa yaachia nyaraka za mauaji ya Rwanda
Faki aliongeza kuwa wanapaswa kuwa na ujasiri na kutambua hilo pamoja na kuwajibika.
Rwanda imeanza wiki moja ya maombolezo
Wakazi wengi waliohudhuria hafla hiyo waliliambia shirika la habari la AFP kwamba wanashiriki historia hiyo ya kusikitisha ya nchi yao, na walipoteza wanafamilia kwenye mauaji hayo.
Hafla hiyo ya jana, iliadhimisha mwanzo wa wiki moja ya maombolezo ya kitaifa ambapo hakuna muziki unaoruhusiwa kupigwa katika maeneo ya umma ama redioni, huku matangazo ya televisheni yakihitajika kuzingatia kile kinachojulikana kama Kwibuka (kumbukumbu ya 30)