Rwanda yaionya DRC dhidi ya uchokozi
29 Desemba 2022Serikali ya Rwanda imeionya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwamba uchokozi wowote unaoendelea kufanywa kwa kutumia ndege za kivita za Kongo kwenye ardhi ya Rwanda ni lazima usitishwe. Rwanda imesema hayo baada ya hapo jana ndege ya kivita ya jeshi la jeshi la Kongo, FARDC kuvuka mpaka na kuingia Rwanda kupitia ziwa Kivu linazozitenganisha nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na serikali ya Rwanda ndege ya kivita ya jeshi la DRC, FARDC aina ya sukhoi 25 iliingia eneo la Rwanda kwenye ziwa Kivu na mara moja kurejea upande wa DRC. Serikali ya Rwanda kupitia tangazo hili imesema hii ni mara ya pili baada ya tukio la tarehe 07 mwezi uliopita ambapo ndege ya kivita ya jeshi la DRC sukhoi 25 vilevile iliingia Rwanda na kutua kwa muda mfupi kwenye uwanja wa ndege wa mjini Rubavu upande wa Rwanda na kisha kuruka tena haraka kurudi DRC.
Serikali ya Rwanda imesema, vitendo hivi ambavyo yenyewe inavitaja kama ni uchokozi unaoendelea ni kinyume kabisa na mikataba ya amani ya Luanda nchini Angola na Nairobi nchini Kenya ambayo kwa pamoja inanuia kuleta suluhu la mzozo wa mashariki mwa DRC.
Ijapokuwa msemaji wa serikali ya Rwanda hakupatikana mara moja kuzungumzia zaidi sakata hili, wiki iliyopita akizungumza kupitia televisheni ya taifa naibu msemaji wa serikali ya Rwanda Alain Mukurarinda alisema ‘'Unaposema unataka amani lakini kwa upande mwingine ukaendelea na vitendo vya uchokozi maana yake una agenda nyingine na sisi hatutavumilia, utawala nchini DRC unaonekana kupewa jeuri na baadhi ya watu kwenye jumuiya ya kimataifa, ambao mara nyingi wanailaumu Rwanda kwa matatizo yote ya DRC huku wakifumbia macho uchokozi dhidi ya Rwanda unaofanywa na serikali ya DRC. Lakini pamoja na hayo sisi tunasema tutaendelea kukaa chonjo na kujiandaa''.
Serikali ya Rwanda imesema kwamba kuendelea kufanya uchokozi kwa misingi ya kuingia kwenye vita vya wazi na jirani yako si jambo linaloweza kutatua mzozo wa DRC na badara yake vitendo hivyo vinaweza kusababisha kuharibika zaidi kwa hali ya usalama.
Wachambuzi kama Paul Muhunde wanasema huenda ujio wa ndege hii ukawa ni matokeo ya uamuzi uliochukuliwa upande wa DRC.
Hali ya sintofahamu baina ya DRC na Rwanda inaendelea kuharibika zaidi kutokana na lawaza kila upande. DRC inailaumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa kundi la M23 ambao tayari wanayashikilia maeneo kadhaa mashariki mwa DRC huku Rwanda ikiilaumu DRC kushirikiana na kundi la wanamgambo wa kihutu wa FDLR ambalo Rwanda inalivisha jukumu la kufanya mauaji ya kimbari kisha kukimbilia mashariki mwa DRC.