Rwanda yakosolewa kwa vitisho na mauaji ya wakosiaji ugenini
10 Oktoba 2023Kulingana na shirika hilo, hayo ni sehemu ya kampeni ya ukandamizaji ambao sharti ukabiliwe na jumuiya ya kimataifa.
Taifa hilo dogo la Afrika Mashariki limeongozwa na rais Paul Kagame tangu mauaji ya halaiki ya 1994 na anapania kuendeleza utawala wake katika uchaguzi mwaka ujao.
Katika ripoti yake mpya iliyochapishwa leo shirika la Human Rights Watch limesema ili kuendeleza udhibiti wa madaraka chama tawala cha Rwandan Patriotic Front kimechukua hatua za kutumia nguvu na machafuko kwa kitisho chochote dhidi ya mamlaka yake.
Shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani pia limesema hatua hizo hazikuwalenga tu wakosoaji na wapinzani ndani ya nchi.
Shirika hilo liliwahoji watu zaidi ya 150 katika ripoti yake inayoijumuisha miaka tangu Kagame alipochaguliwa katika uchaguzi wa 2017.