1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

S. Kusini wakubaliana kuunda serikali Feb. 2020

17 Desemba 2019

Salva Kiir na Riek Machar wamekubaliana kuunda serikali ya pamoja kufikia muda wa mwisho wa Februari 2020, wakati shinikizo la kimataifa dhidi yao likizidi juu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Septemba 2018.

https://p.dw.com/p/3Uxp3
Südsudan Präsident Salva Kiir und Vizepräsident Riek Machar
Picha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Siku ya Jumanne (17 Novemba) Rais Kiir aliarifu kwamba yeye na kiongozi wa upinzani, Machar, walikuwa wamefikia makubaliano hayo, baada ya wawili hao kukutana kwa siku tatu mfululizo katika mji mkuu, Juba.

Kiir alisema lengo la mazungumzo yao lilikuwa ni kutatuwa mizozo iliyozuwia kuundwa kwa serikali hiyo pale muda wa mwisho ulipofika, tarehe 12 Novemba. 

Kumekuwa na wasiwasi kutoka jumuiya ya kimataifa kwamba pande hizo mbili zinaweza kurejea kwenye vita endapo tafauti baina yao hazikutatuliwa. 

Mnamo Oktoba 2019, viongozi hao wawili walijiongezea tena muda kwa kuchelewesha uundaji wa serikali mpya kwa siku 100 zaidi, nje kabisa ya muda wa mwisho uliowekwa. Na hiyo haikuwa mara ya kwanza kuchukuwa hatua ya kuakhirisha kuunda serikali baada ya makubaliano ya Septemba 2018. 

"Tumesema kwamba baada ya siku 100 hizi, lazima tuwe tumeshaunda serikali," alisema Kiir, akiongeza kwamba mazungumzo mengine yoyote yaliyosalia yataendelezwa na serikali hiyo mpya itakayoundwa. 

Marekani yawawekea vikwazo mawaziri wa Kiir

USA Washington | Außenminister Mike Pompeo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, alitangaza vipya kwa mawaziri wawili wa serikali ya Sudan Kusini kwa sababu ya kuzuwia uundwaji wa serikali ya pamoja.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Brandon

Kiir alitangaza makubaliano yake hayo na Machar siku moja tu baada ya Marekani kutangaza vikwazo vipya kwa mawaziri wake wawili, ikiwatuhumu kwa kuzuiwa utaratibu wa kufikiwa amani ya kudumu nchini Sudan Kusini, licha ya ahadi ya kuundwa kwa serikali hiyo ya pamoja.

Amri ya Jumatatu (Novemba 16) ya Marekani ilimuhusu Waziri wa Ulinzi, Koul Manyang Juuk, na Waziri wa Mambo ya Utawala, Martin Elia Lomuro, ambao wote walipigwa marufuku kuingia Marekani na mali zao zimezuiliwa.

Taarifa ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo, ilisema raia wa Sudan Kusini "wanahitaji kuwa na viongozi waliojitolea kujenga misingi kwa ajili ya kipindi cha mpito cha kisiasa kilicho cha amani na chenye mafanikio."

Hiyo ilikuwa hatua nyengine kubwa kutoka Marekani, ambayo imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Sudan Kusini.

Awali, Marekani ilikuwa imemuita nyumbani balozi wake nchini Sudan Kusini kwa mashauriano, ingawa ilisema isingelikata msaada wake wa takribani dola bilioni moja kwa nchi hiyo, ambao hutumika kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine ya kibinaadamu.

Sudan Kusini ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, miaka miwili tu baada ya kupata uhuru kutoa Sudan, kufuatia mzozo baina ya Kiir na Machar, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni.

Makubaliano kadhaa ya amani na jitihada za upatanishi zimeshindwa kuleta amani kwenye taifa hilo changa kabisa duniani. 

Hata hivyo, makubaliano hayo ya mwaka 2018 yalifanikiwa kusitisha kuendelea kwa mauaji, lakini ilikuwa ni baada ya watu 400,000 kupoteza maisha na wengine milioni nne - ambao ni sawa na robo nzima ya raia wote - kugeuka wakimbizi.