1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sakata la busu laendelea Uhispania

29 Agosti 2023

Marais wa mikoa ya shirikisho la soka la Uhisapania (RFEF) wamemtaka Luis Rubiales kujiuzulu mara moja kutoka nafasi ya rais wa shirikisho.

https://p.dw.com/p/4VhOv
Präsident des Spanischen Fußballverbande sLuis Rubiales gibt Kuss an Spielerin Jennifer Hermoso
Picha: AFP

Rubiales amekataa kujiuzulu licha ya kuibua hasira baada ya kumbusu mchezaji wa Uhispania Jenni Hermoso mdomoni wakati wa uwasilishaji wa Kombe la Dunia la wanawake mnamo Agosti 20.

Soma pia: FIFA yamsimamisha rais wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales

Baada ya kikao kilichofanyika Jumatatu jioni, Kamati ya Marais ya Mashirikisho yanayojiendesha ya Kieneo ya RFEF yalisema tukio hilo "limeharibu sana taswira" ya soka la Uhispania.

"Kamati ya Marais wa mikoa inamwomba Bw. Luis Rubiales kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwake kama rais wa RFEF mara moja," taarifa ilisema.

Aidha marais hao wametoa wito wa kutaka marekebisho katika usimamizi wa Shirikisho la Soka la Uhispania, RFEF, na kwa kauli moja kumuunga mkono rais wa mpito Pedro Rocha, ambaye alichukua madaraka baada ya Rubiales kusimamishwa kazi kwa muda na Shirikisho la soka duniani FIFA.

Mashtaka katika mahakama ya Madrid

Kombo | Hermoso und Rubiales
Rubiales na HermosoPicha: John Cowpland/Rfef/EUROPA PRESS/AP/dpa/picture alliance

Wakati haya yakijiri, waendesha mashtaka wa Madrid wamezindua uchunguzi juu ya kesi ya awali ya kashfa ya busu na watamuuliza Jenni Hermoso kama anataka kufungua mashtaka dhidi ya Rubiales.

Hata hivyo kutokana na kuwa tukio hilo lililotokea katika mji wa Sydney nchini Australia ushiriki wa waendesha mashtaka wa Uhispania unaweza kuwa mgumu. Lakini msemaji wa mahakama ya Uhispania amesema kwamba  "kulingana na kauli wazi kwa umma " za Hermoso, mwenye umri wa miaka 33, anaweza kuwa mwathirika wa madai ya unyanyasaji wa kijinsia, kama inavyoonekana kuwa "hakukuwa na aina yoyote ya kukubali."

Soma pia: Rais wa soka wa Uhispania agoma kujiuzulu kwa kosa la busu

Kituo cha redio cha Cadena Ser kiliripoti kwamba Hermoso ana siku 15 za kuwasilisha mashtaka.

Waendesha mashtaka wanaweza pia kuwa wanatafuta kuona ikiwa Rubiales amevunja Sheria nyengine za Uhispania. Alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Hermoso na kumshutumu kwa kusema uwongo kwamba busu hilo halikuwa la makubaliano.

Rubiales amefungiwa na FIFA kwa siku 90 kusubiri matokeo ya uchunguzi wakati serikali ya Uhispania imepeleka kesi katika mahakama ya michezo, ambayo ilikutana kwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu.

Víctor Francos, rais wa Baraza la Michezo la Juu la serikali ambayo ilipeleka kesi kwenye mahakama ya michezo, iliambia mkutano wa wanahabari kwamba "Tunaendelea kuamini kuwa malalamiko yetu yana mashiko yote ya kisheria kushughulikiwa kwa umakini sana."

Umoja wa Mataifa umelaani vitendo vya Rubiales, wakisema kwamba hakukuwa na dalili kwamba busu hilo lilikuwa la makubaliano.

"Je, ni vigumu kwa kiasi gani kutombusu mtu midomo?" alisema Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katika mkutano na waandishi wa habari.

Tuko pamoja na wewe Jenni

Timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania ilitia saini barua ya pamoja na Hermoso ikisema kuwa hawatawakilisha tena nchi yao iwapo uongozi wa sasa wa shirikisho la kandanda hautaondolewa. Timu hiyo  tayari haikuwa na uhusiano mzuri naye baada ya kuungana na kocha Jorge Vilda katika mzozo na timu hiyo kabla ya michuano ya wanawake ya Kombe la Dunia.

Mexiko l Rücktrittsforderung an Rubiales l Frauenfußballvereins Pachuca zeigt Soldiarität mit Jenni
Wachezaji wa timu ya Pachuca wakiwa na bango lilioandika "Tuko pamoja na wewe Jenni."Picha: Christian Chavez/AP/picture alliance

Wacheza kandanda wanawake ulimwenguni kote wameonyesha mshikamano kwa Hermoso katika wiki iliyopita.

Kwa sasa, shirikisho la soka la Ulaya UEFA limeachia mamlaka kwa FIFA, kutokana na tukio la kumbusu lililotokea wakati wa Kombe la Dunia. Kwa mujibu wa taarifa za dpa, mabaraza yote mawili ya uongozi yamekuwa yakijadili hatua zitakazochukuliwa.

Rubiales amekuwa kwenye Kamati ya Utendaji ya UEFA kama makamu wa rais tangu 2019. Kufikia sasa, hakuna afisa mkuu wa UEFA ambaye ametoa maoni kuhusu kashfa hiyo.

Damu ni nzito kuliko maji

Präsident des spanischen Fußballverbandes Luis Rubiales
Picha: Óscar J.Barroso/AFP/dpa/picture alliance

Wakati huo huo, ripoti za vyombo vya habari vimeripoti kwamba mamake Rubiales alikuwa kwenye mgomo wa kula na alikuwa amejifungia kanisani kupinga kashfa dhidi ya mwanawe.

Mamake mwenye umri wa miaka 46 alijifungia katika kanisa la Andalusian katika mji wa Motril kusini mwa Uhispania katika kile alichokiita "uhasama wa kinyama " dhidi ya mtoto wake na kulingana na ripoti alitaka kuendelea na mgomo wa kula "siku na usiku" mpaka "haki itakapotendeka."

Makumi ya watu walikusanyika mbele ya kanisa hilo katika kuonyesha mshikamano na kumuunga mkono Rubiales.

Uhispania ilishinda 1-0 dhidi ya England kwenye fainali mnamo Agosti 20, ushindi wa kwanza wa Kombe la Dunia kwa wanawake kwa taifa hilo ambao badala yake umegubikwa na kashfa.

 

//dpa//https://p.dw.com/p/4Vg1g