Saudi Arabia na washirika wake wanajadili mzozo wa Qatar
5 Julai 2017Saudi Arabia, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri mapema leo zimesema zimepokea jibu la Qatar na kwamba watalishughulikia kwa wakati muafaka. Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo nne zilizositisha uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara na Qatar wanakutana leo kujadili jinsi ya kuushughulikia mzozo huo.
Qatar yaapa kutosalimu amri
Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani aliwasilisha mtizamo rasmi wa nchi yake kwa Kuwait ambayo ni mpatanishi wa mzozo huo wa ghuba kwa kusema kuwa orodha ya masharti ambayo nchi yake inapaswa kutimiza hayawezi kutekelezeka na hayahusu vita dhidi ya ugaidi bali yanalenga kuzima uhuru wa kujieleza.
Sheikh Mohammed amesema Qatar haitasalimu amri na kuwa orodha ya masharti 13 iliyowekewa hayatekelezeki na yalikusudiwa kukatiliwa. Hata hivyo ameongeza kusema kuwa wanatafuta suluhisho kwa mzozo huo kupitia mazungumzo. Nchi hiyo inashutumiwa kwa kuunga mkono ugaidi, madai ambayo imeyakanusha vikali.
Miongoni mwa masharti hayo ni Qatar kukoma kuunga mkono udugu wa Kiislamu, kukifunga kituo cha televisheni cha Al Jazeera, kupunguza uhusiano wa kidiplomasia na Iran na kuifunga kambi ya kijeshi ya Uturuki iliyoko nchini humo. Saudi Arabia na washirika wake zimetishia kuiwekea Qatar vikwazo zaidi iwapo haitatimiza masharti iliyowekewa.
Ujerumani yajitolea kusaidia
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye jana alihitimisha ziara ya siku tatu katika eneo hilo la ghuba amesema Qatar imeonyesha kujizuia katika mzozo huo na kutoa wito majirani zake pia kuchukua mtizamo huo ili mzozo huo usizidi kuwa mbaya zaidi.
Akizungumza na wanahabari mjini Doha jana wakiwa na mwenyeji wake Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al Thani, Gabriel amesema Ujerumani na Umoja wa Ulaya ziko tayari kusaidia kuutatua mzozo huo kupitia mazungumzo kwani Ujerumani ina maslahi yake katika kanda hiyo na ingependa kuyalinda.
Mzozo huo wa ghuba umeibua wasiwasi wa kusababisha msukosuko katika kanda hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi na ambako nchi kadhaa za magharibi zina kambi zake za kijeshi. Qatar ndiyo mzalishaji mkubwa duniani wa gesi na raslimali hiyo imeifanya nchi hiyo kuwa mojawapo ya nchi tajiri zaidi duniani, mwekezaji mkubwa na mojawapo ya nchi zilizo na ushawishi mkubwa katika kanda hiyo.
Qatar pia inafuata sera huru za kigeni kinyume na majirani zake ambao hufuata mkondo wa nchi yenye nguvu zaidi ya ghuba Saudi Arabia.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Josephat Charo