Saudi Arabia ni mshirika wa Magharibi au mfadhili wa ugaidi?
8 Agosti 2011Rais wa Marekani Barack Obama alifanya ziara yake ya kwanza katika Mashariki ya Kati Juni mwaka 2009, muda mfupi baada ya kushika wadhifa wake mpya. Nchini Saudi Arabia, alikuwa na sifa nyingi kuhusu nchi hiyo ya kifalme. Alisisitiza kuwa nchi hizo mbili sio washirika wa kibiashara tu, bali ni washirika wa kimkakati vile vile.
Lakini ikiwa hati za siri zilizofichuliwa na tovuti ya Wikileaks zinaaminika, basi mwaka huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, alikuwa na maoni tofauti. Kwani kwa mujibu wa nyaraka za mawasiliano ya serikali zilizofichuliwa, kwa ghadhabu Clinton aliandika kuwa "ni changamoto isiyo na mwisho kuwashawishi maafisa wa Saudi Arabia kwamba suala la michango ya fedha inayosaidia ugaidi, linahitaji kupewa kipaumbele".
Lawama hizo zilifikia kilele ilipojulikana kuwa Saudi Arabia ina umuhimu mkubwa kama kitovu cha michango hiyo ya fedha kwa makundi ya kigaidi kote ulimwenguni. Suali linalozuka hapa ni ikiwa je, Saudi Arabia inaangalia vipi na Ikulu ya Marekani linapokuja suala la vita dhidi ya ugaidi duniani: kama mshirika wa kimkakati au mfadhili wa magaidi?
Saudi Arabia, Marekani na uhusiano wa mashaka
Kutafautiana kimatamshi kati ya rais wa Marekani na waziri wake wa mambo ya nje kunaonyesha jinsi uhusiano kati ya nchi hiyo na Saudi Arabia ulivyo na utata. Kwa upande mmoja, Saudi Arabia sio tu muuzaji muhimu kabisa wa mafuta kwa Marekani katika Mashariki ya Kati, bali pia inathaminiwa na Marekani kama mshirika muhimu dhidi ya ushawishi wa Iran unaoenea na vile vile kama nchi inayoshiriki katika jitahada za kidiplomasia kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya kanda hiyo. Kwa upande mwingine, huko Saudi Arabia kuna mambo mengi ambayo katika nchi nyingine hukosolewa vikali na Marekani: ukiukwaji wa haki za binadamu, uhaba wa uhuru wa dini, uchujaji wa habari, ukosefu wa usawa baina ya wanaume na wanawake. Mengi ya hayo yana msingi wa itikadi za madhehebu ya Wahabi, ambayo ni maarufu kwa itikadi kali za Kiislamu. Kwa hivyo, wataalamu wengi wala hawakushtuka kuwa sehemu kubwa ya washambuliaji wa Septemba 11 walitokea Saudi Arabia.
Mfalme Abdullah kwa hadhari anajaribu kufanya mageuzi. Lakini Guido Steinberg, mtaalamu wa masuala ya Uislamu katika taasisi ya sayansi na siasa mjini Berlin anasema kuwa itikadi za madhehebu ya Wahabi na zile za al-Qaida zinafanana katika mambo mengi. "Kwa hivyo, ni rahisi kwa vijana wa Saudi Arabia kutumbukia katika mazingira ya al-Qaida, ingawa viongozi wa Saudi Arabia hawataki kukubali kuwa itikadi zao na zile za al-Qaida zinakaribiana." Ndivyo anavyoamini Steinberg.
Fedha za magaidi hazitoki Saudi Arabia tu
Lawama kubwa kabisa dhidi ya Saudi Arabia inahusika na fedha zinazosaidia ugaidi, ingawa bado haijathibitishwa iwapo ni kweli kuwa sehemu kubwa ya michango ya al-Qaida hutoka Saudi Arabia na nchi zingine za Ghuba. Yassin Musharbash wa jarida la Kijerumani, Der Spiegel, anaamini kuwa mara kwa mara, watu husafiri na mikoba iliyojaa fedha kutoka Saudi Arabia kwenda Afghanistan au Pakistan "na fedha hizo huishia katika kambi za kigaidi au kambi za mafunzo". Musharbash anasema, maafisa wa Saudi Arabia hawawezi kulaumiwa, kwani kwa sehemu fulani mtandao wa mashirika ya misaada, kwa makusudi, hutumiwa vibaya bila ya wenyewe kujua.
Hata hivyo, al-Qaida haipati fedha kutoka kwa matajiri wa Kisaudi na wa nchi zingine za Ghuba tu. Musharbash anaeleza kuwa kwa muda mrefu makundi ya kigaidi yamekuwa yakitumia mtandao wa intaneti na mitandao ya binafsi, kukusanya fedha kutoka kwa wafuasi wake kila pembe ya dunia.
Vile vile, wanamgambo wa al-Qaeda waliopiga kambi katika kanda ya Maghreb wamegundua njia nyingine ya kupata fedha: wanamgambo hao huteka nyara watu na hasa raia wa kigeni ili kupata fedha za kuwagomboa.
Mwandishi: Khalid El Kaoutit/ZPR
Tafsiri: Prema Martin