1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Save the Children: Watoto bilioni 1.2 hatarini

31 Mei 2018

Takriban watoto bilioni 1.2 duniani kote wanakabiliwa na hatari kubwa ya kutumbukia kwenye umasikini hayo yamechapishwa kwenye ripoti mpya ya Shirika la kutetea Haki za Watoto.

https://p.dw.com/p/2yhhy
Niger Symbolbild Kinderehe
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Shirika hilo limesema nusu ya idadi ya watoto kote duniani wanakabiliwa na kitisho hicho kutokana na migogoro. Kulingana na Shirika lisilokuwa la kiserikali la kutetea haki za watoto la Save the Children, hali ya watoto wa Ulaya ni bora ikilinganishwa na hali ya watoto walio katika bara la Afrika ambayo sio ya kupendeza. 

Miongoni mwa hatari zinazowakabili watoto hao ni pamoja na kulazimishwa kufanya kazi, kunyimwa elimu, mimba za mapema, ndoa za utotoni, na ubaguzi dhidi ya mtoto wa kike huku machafuko ya kila mara yakiwa ndio chanzo cha kuviongeza vitisho hivyo.

Ripoti hiyo imesema, kati ya nchi nyingi zilizoorodheshwa kuwa na mazingira magumu kwa watoto ni pamoja na za Afrika ya Kati na Afrika Magharibi. Niger ikiwa ndiyo ya mwisho kabisa katika orodha hiyo na bila kuziacha mbali nchi za Mali na Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Mtoto wa Syria
Mtoto wa Syria Picha: picture-alliance/dpa/Save the children

Singapore na Slovenia zilichukua nafasi ya kwanza kuhusiana na ubora wa mazingira kwa watoto. Ujerumani iko katika nafasi ya 12, huku Marekani ikiwa inashikilia nafasi ya 36 ikifuatiwa na Urusi katika nafasi ya 37.

Nchi nyingine saba za Ulaya Magharibi pia zimeorodheshwa kwenye idadi ya nchi kumi bora kwa kupata alama za juu kutokana na jitihada zao katika kushughulikia afya ya watoto, elimu na kuwalinda watoto, hayo yamechapishwa kwenye ripoti hiyo mpya iliyotolewa hapo jana Jumatano.

Kati ya nchi 175 zilizoorodheshwa kwenye utafiti huo, 95 zilionyesha kupiga hatua katika kupambana na mojawapo ya hatari zinazowakabili watoto. Shirika la kutetea haki za watoto katika ripoti yake hiyo limependekeza kwamba jumuiya ya kimataifa ichukue hatua na kutumia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo Endelevu (SDG) kama njia ya kuhakikisha usalama wa watoto duniani kote.

Mama na Mtoto  huko nchini Senegal
Mama na Mtoto huko nchini SenegalPicha: imago/i Images/A. Parsons

Shirika hilo limetoa wito kwa viongozi ulimwenguni kuzingatia thamani ya watoto na haki yao ya kuishi, kukua na kulindwa kwa kufuata ahadi zilizofikiwa kwenye makubaliano ya mpango Maendeleo Endelevu wa Umoja wa Mataifa kwa kuchukua hatua za haraka kutekeleza ahadi ya kutokumwacha mtu yeyote nyuma.

Shirika hilo limesema mbali na dhamana hizi za kimataifa, hatua maalum zinahitajika kuchukuliwa ili kushughulikia umasikini, migogoro na ubaguzi wa jinsia, huku lengo kuu likiwa ni wasichana na watoto ambao ni wakimbizi. Shirika hilo la Save The Children limebainisha kuwa matatizo wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua ni sabbau moja kubwa ya vifo kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 19 duniani kote.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/p.dw.com/p/2ygA6

Mhariri:Yusuf Saumu